Wanawake nchini Afghanistan waunga mkono Hijabu na Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74496-wanawake_nchini_afghanistan_waunga_mkono_hijabu_na_taliban
Mamia ya wanawake nchini Afghanistan wamekusanyika katika mkoa wa Kunduz kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo sambamba na kutangaza uungaji mkono wao kwa Taliban wamesisitizia pia uvaaji wa vazi la stara la Kiislamu la Hijabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 10, 2021 08:12 UTC
  • Wanawake nchini Afghanistan waunga mkono Hijabu na Taliban

Mamia ya wanawake nchini Afghanistan wamekusanyika katika mkoa wa Kunduz kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo sambamba na kutangaza uungaji mkono wao kwa Taliban wamesisitizia pia uvaaji wa vazi la stara la Kiislamu la Hijabu.

Katika mkusanyiko wao huo, wanawake wa Kiafghani mkoani Kunduz wametoa nara na shaa'r za "sisi tunataka dada zetu wote waishi chini ya mwamvuli wa Hijabu ya Kiislamu".

Wanawake hao Waislamu wa Afghanistan aidha wamesikika wakitoa nara na kaulimbiu za "sisi tunataka Mfumo wa Kiislamu si demokrasia; tunataka dini ya Uislamu; na mauti kwa watu waliowafanya dada zetu wasiwe na Hijabu."

Kabla ya mkusanyiko huo wa Kunduz, wanawake wa Afghanistan walikusanyika pia katika mji mkuu Kabul, wakitaka Muhammad Ashraf Ghani, rais wa nchi hiyo aliyekimbilia nje ya nchi ashtakiwe na vilevile kuchungwa haki za wanawake katika utawala wa Taliban katika nyuga na nyanja zote.

Zabihullah Mujahid

Kundi la Taliban, ambalo limeshika hatamu za utawala nchini Afghanistan baada ya kuuteka mji mkuu Kabul mnamo tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Agosti, limekuwa likisisitiza kuwa, wanawake wa Afghanistan wataweza kufanya shughuli zao na kuendelea na masomo kwa mujibu wa sharia za Uislamu.

Alipozungumza katika mahojiano aliyofanyiwa hivi karibuni, msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid alisema, kwa mujibu wa hukumu za Qur'ani na sharia za dini, wanawake hawawezi kushika wadhifa wa uwaziri katika utawala wa kundi hilo, lakini hakuna kizuizi chochote kwa wao kufanya kazi katika sekta za tiba na elimu.../