Serikali ya Canada yahukumiwa kuwalipa fidia wakazi asili wa nchi hiyo
Mahakama ya Haki za Binadamu ya Canada ambayo mwaka 2016 iliituhumu serikali ya nchi kuwa imefanya ubaguzi wa kimbari, kutumia mabavu na kuua Wahindi Wekundu wenyeji wa nchi hiyo imeitaka serikali ya Ottawa kuwalipa fidia Wahindi Wekundu kwa kupatikana na hatia ya kukiuka haki zao za kibinadamu
Serikali ya Waziri Mkuu, Justin Trudeau ambayo mwaka 2019 ilikata rufaa ikipinga hukumu kama hiyo, mara hii pia imehukumiwa kulipa fidia ya dola elfu 40 kwa kila familia ya Mhindi Mwekundu aliyefanyiwa ukatili ili kufidia hasara za mauaji na siasa zake za kibaguzi. Inatazamiwa kuwa, hukumu hiyo itaigharimu mabilioni ya dola serikali ya federali ya Canada.
Hukumu ya mahakama hiyo ya Canada kwa hakika inathibitisha tuhuma zilizotolewa kwa miaka mingi kuhusu ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifanywa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya Wahindi Wekundu wenyeji wa nchi hiyo.
Wahidi Wekundu wa Canada (Aboriginals) ndio wakazi asili na wenyeji wa nchi hiyo kabla ya Canada haijagunduliwa katika karne ya 15, na hadi sasa wangali wanaishi katika mipaka ya ardhi ya nchi hiyo na wanajumuisha kaumu za First Nations, The Inuit na The Metis.
Takwimu zinaonesha kuwa, Canada ina zaidi ya Wahindi Wekundu milioni moja na laki mbili, na jamii yao inaishi katika hali mbaya ikisumbuliwa na kiwango cha juu ya umaskini, kujiua na uraibu wa dawa za kulevya. Hii ina maana kwamba, jamii hiyo ya wenyeji inasumbuliwa na matatizo mengi yanayotokana na siasa za ubaguzi wa kimbari za serikali ya Canada. Watu wa jamii hii wamekuwa wakiishi katika sulubu na ukandamizaji mkubwa wa wazungu na serikali ya Ottawa kwa karne kadhaa sasa.
Wakati huo huo sasa imebainika kwamba, Kanisa Katoliki pia limehusika pakubwa katika ukandamizaji na mienendo ya kikatili dhidi ya watoto wa wenyeji hao wa Canada waliotenganishwa kwa mabavu na wazazi wao na kushikiliwa katika shule za bweni za wamishonari. Asasi na mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu zinaituhumu serikali na Canada na Kanisa Katoliki kwa kushirikiana katika kuwakandamiza wenyeji wa nchi hiyo, kukiuka haki zao za binadamu, mienendo ya kibaguzi na kukanyaga sheria za kimataifa.
Mienendo ya kibaguzi ya serikali ya Canada dhidi ya wenyeji na wakazi asili wa nchi hiyo imeendelea pia katika karne ya 21 na kukabiliwa na upinzani mkubwa wa mashirika na jumuiya za kutetea haki za binadamu. Ripoti ya karibuni ya shirika la Amnesty International ilitangaza kuwa, kuwatenga na kutowashirikisha wakazi asili na wenyeji wa Canada katika uchukuaji wa maamuzi ya nchi kunaifanya Canada iwe mbali na vigezo vya haki za binadamu vilivyotangazwa katika Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wakazi asilia na wenyeji.
Ripoti iliyotolewa mwaka 2018 na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa iliashiria vipengee vya kibaguzi vilivyoko katika “Sheria ya Wenyeji” (Aboriginal Law) nchini Canada. Ripoti hiyo imesema kuwa, Canada inapaswa kufuta vipengee hivyo vya kibaguzi. Sheria hiyo ilibuniwa mwaka 1876 kwa misingi ya ubaguzi.
Moja kati ya vielelezo vya mienendo ya kikatili iliyofanywa dhidi ya wenyeji na wakazi hao asili wa Canada ni makumi ya makaburi ya umati ya jamii ya watu hao yaliyogunduliwa nchini humo. Katika miezi kadhaa ya karibuni pekee makuburi kadhaa ya umati yaliyokua na maiti za mamia ya watoto wa wenyeji hao wa Canada waliokuwa wakishikiliwa katika shule za bweni wa wamishonari wa Kikatoliki yamegunduliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Watoto hao walitenganishwa kwa mabavu na wazai wao na kushikiliwa katika shule hio za wamishonari wa kizungu kwa shabaha ya kubadili utambulisho na utamaduni wao.
Kugunduliwa kwa makaburi hayo ya umati yanayofikia 200 yenye miili ya maelfu ya watoto wa Wahindi Wekundu ni ithibati kwamba, wenyeji hao wa Canada wamekuwa wakisumbuliwa na ubaguzi wa kimfumo na wa kupanga tangu wahamiaji wazungu kutoka Ulaya walipohamia huko America ya Kaskazini, na baguzi huo wa kimfumo bado unaendelea hadi hii leo.
Japokuwa Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amefanya jitihada za kufunika fedheha ya kugunduliwa mamia ya makaburi ya umati yenye maelfu ya maiti za watoto wa wenyeji hao kwa kuwapa watu wa jamii hiyo aina flani ya mamlaka, lakini ukweli ni kuwa jinai hiyo ni kubwa mno na imekita mizizi katika historia ya Canada kiasi kwamba, si rahisi kuifuta kwa hatua kama hizo za kipropaganda.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wenyeji wa Canada, Perry Belgerd ameashiria ukweli huo mchungu akisema kuwa kugunduliwa makaburi ya umati ya wanafunzi wa shule za bweni za wamishonari nchini Canada si jambo jipya na kwamba ni jeraha la miaka mingi ambalo kufunuliwa kwake daima huambatana na maumivu makali.
Haya yote na licha ya kuwa, Canada imekuwa ikijigamba kuwa mtetezi wa haki za binadamu na daima imekuwa ikijitokeza katika majukwaa ya kimataifa kama Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuzituhumu nchi inazopinga sera za kibeberu za Wamagharibi.
Alaa kulli hal, faili la haki za binadamu la Canada lina nukta nyingi za giza ikiwa ni pamoja na mienendo ya kikatili ya serikali ya nchi hiyo dhidi ya wenyeji na wakazi asili.