Waislamu Marekani watoa wito wa kukomeshwa ujasusi dhidi ya jamii yao
(last modified Fri, 31 Dec 2021 08:18:24 GMT )
Dec 31, 2021 08:18 UTC
  • Waislamu Marekani watoa wito wa kukomeshwa ujasusi dhidi ya jamii yao

Kundi kubwa la kutetea haki za Waislamu nchini Marekani limetoa wito wa kusitishwa ujasusi unaofanya dhidi ya jamii ya wafuasi wa dini hiyo na kuchukuliwa hatua kali kwa wahusika wa vitendo hiyo.

Ni baada ya kufichuliwa habari zaidi za ujasusi unaofanywa dhidi ya taasisi za Kiislamu za Marekani ikiwemo misikiti ambazo zinakabidhiwa kwa makundi yanayopiga vita Uislamu na ya Kizayuni.

Ujasusi huo uliofichuliwa mapema mwezi huu na Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) umewatikisa mawakili wa Kiislamu nchini humo na kuibua upya wasiwasi wa muda mrefu kuhusu ujasusi unaofanywa dhidi ya jamii ya Waislamu wa Marekani.

Mkurugenzi wa masuala ya jamii katika jumuiya ya CAIR huko Ohio, Whitney Siddiqi, amesema: "Wanajamii wameshtushwa na kuhuzunishwa na hali hii, lakini watu wengi pia hawakushangaa kwamba kundi lenye chuki dhidi ya Uislamu lilikuwa likilenga jumuiya za Kiislamu ikiwemo CAIR na kufanya ujasusi."

Mnamo Desemba 15 CAIR ilitangaza kwamba imemfuta kazi Romin Iqbal, mkurugenzi wake mtendaji katika eneo la Columbus-Cincinnati, kwa "ukiukaji mkubwa wa maadili na kitaaluma".

CAIR ilimtuhumu Iqbal kwa kutoa taarifa za siri kwa kundi linalojiita Investigative Project on Terrorism (IPT), ambalo shirika la kutetea haki za kiraia linalofuatilia makundi yanayochochea chuki nchini Marekani (SPLC), limesema lilianzishwa na mwanaharakati anayepiga vita Uislamu.

Ushahidi unaonesha kuwa, genge hilo lina ushirikiano wa karibu na shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags