UN: Kutunza Mazingira ni msingi wa amani, maendeleo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i7888-un_kutunza_mazingira_ni_msingi_wa_amani_maendeleo
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson , amesema kutunza mazingira ni msingi wa amani, maendeleo na ubinadamu kwa wote.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 27, 2016 03:31 UTC
  • Jan Eliasson
    Jan Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson , amesema kutunza mazingira ni msingi wa amani, maendeleo na ubinadamu kwa wote.

Amesema hayo Alkhamisi akihutubia mkutano wa pili wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEA, unaoendelea wiki hii huko Nairobi, Kenya.

Eliasson ameongeza kwamba ni lazima kuchukua hatua mapema na kwa ushirikiano, ili kudhibiti madhara ya mabadiliko ya tabianchi, akizingatia umuhimu wa ubia wa kimataifa.

Ameongeza kuwa, kuachana na mafuta ya petroli kutakuwa vigumu hata kama wote wanafahamu kwamba suluhu mbadala zipo.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema bado kuna fikra duni kwamba tunapaswa kuchagua baina ya ukuaji wa uchumi na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema Afrika ndio bara linaloweza kunufaika zaidi kutokana na juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, akitumai nchi nyingi zaidi zitapatia kipaumbele suala hilo.

Mkutano huo wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEA umewaleta pamoja wajumbe zaidi ya elfu moja kutoka kote duniani. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawakilishwa na Makamu wa Rais na Mkuu wa Shirika la Kulinda Mazingira Bi. Masoumeh Ebtekar.