Cuba yalaani jinai za Marekani katika Hori ya Guantanamo
(last modified Wed, 12 Jan 2022 15:36:05 GMT )
Jan 12, 2022 15:36 UTC
  • Cuba yalaani jinai za Marekani katika Hori ya Guantanamo

Cuba imelaani kuendelea kuwepo Jeshi la Marekani katika Hori ya Guantanamo iliyo mashariki mwa nchi hiyo ya Amerika ya Latini, huku ukiwa umewadia mwaka wa 20 tokea gereza la kugofya la Marekani lifunguliwe katika eneo hilo.

Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumanne, Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel amesema:  "Ni miaka 20 sasa ya kashfa ya mateso katika ardhi ya Cuba ya Hori ya Guantanamo inayokaliwa kwa mabavu na wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu duniani."

Ujumbe huo wa Twitter umeandamana na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ambao Jumatatu walitoa taarifa ya kulaani kuendelea kuwepo jela hiyo ya kijeshi ya Marekani hapo Guantanamo huku wakitaka ifungwe mara moja.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodrigue Parilla pia ametaka Marekani ifunge jela hiyo ya kuogofya mara moja. Amesema: "Kituo cha Jeshi la Marekani Guantanamo kina historia ya miaka 20 ya kuaibisha ambapo watu 780 wamewahi kushikiliwa hapo bila kufunguliwa mashitaka wakiwemo watoto.

Wafungwa wakiwa katika jela ya Guantanamo Bay ya Jeshi la Marekani katika ardhi ya Cuba inayokaliwa kwa mabavu

Hivi karibuni Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito kwa Rais Joe Biden likimtaka atekeleze ahadi yake ya kufunga jela ya Guantanamo. 

Amnesty International imetoa wito huo kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya miaka ishirini tangu kuanzishwa jela hiyo ya kutisha ya Guantanamo. Wafungwa 39 wangali wanashikiliwa katika jela hiyo, akiwemo Khalid Sheikh Mohammed, anayeshukiwa kupanga mashambulizi ya 9/11 dhidi ya minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York. Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, mwaka 2009 alisaini amri ya utekelezaji ya kufungwa gereza hilo, lakini alishindwa kufanikisha mchakato huo wakati wa uongozi wake. Cuba inasisitiza kuwa Marekani inakalia kwa mabavu eneo la Hori ya Guantanamo kinyume cha sheria za kimataifa.