Denmark yawapata na hatia magaidi wafanya ujajusi wa Saudia
Mahakama moja nchini Denmark imewapata na hatia ya kufanya ujasusi kwa niaba ya Saudi Arabia wanachama wa kundi la kigaidi la Ahvaziyyah, na kuunga mkono harakati za ugaidi nchini Iran.
Tovuti ya habari ya Ritzau ya Denmark iliripoti hayo jana Ijumaa na kufafanua kuwa, wanachama watatu wa kundi la kigaidi ambalo linajiita Harakati ya Mapambano ya Waarabu kwa ajili ya Ukombozi wa Ahvaz (ASMLA) wamepatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa niaba ya Riyadh.
Aidha wanachama hao wa Ahvaziyyah wamepatikana na hatia ya kuunga mkono mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sambamba na kulinga mkono genge la kigaidi la Jaish ul-Adl.
Majasusi hao wa Saudia ambao walitiwa mbaroni miaka miwili iliyopita, wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 12 jela kwa makosa hayo, pamoja na kosa la kupeana taarifa za Denmark na mashirika ya kigeni na watu binafsi kwa Idara ya Ujasusi ya Saudia. Yumkini pia wakapokonywa uraia wa Denmark na kutimuliwa katika nchi hiyo ya Ulaya.
Itakumbukwa kuwa, mnamo Septemba mwaka 2018, watu 25 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa katika shambulio la kinyama la kigaidi lililofanywa na wanachama wa kundi hilo mjini Ahvaz, kusini magharibi mwa Iran.
Magaidi hao wenye silaha waliwafyatulia risasi wananchi waliokuwa wakitazama gwaride la vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lililokuwa likifanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu, ambapo askari kadhaa pia waliuawa.