China: Sifa ya utumiaji mabavu inaistahiki Marekani peke yake
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amesema, sifa ya utumiaji mabavu inaistahiki Marekani peke yake.
Mivutano baina ya Marekani na China imefikia kiwango ambacho katika mikutano yao ya kila siku na waandishi wa habari, wasemaji wa wizara za mambo ya nje za nchi hizo mbili huwa hawakosi kugusia japo maudhui moja inayolenga kukosoa hatua za upande wa pili pamoja na sera zake.
Katika mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian amejibu kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliyeituhumu Beijing kuwa inatumia mabavu ya kiuchumi dhidi ya Australia na kusema, nchi kama Marekani tu ndiyo inayostahiki sifa kama hiyo.
Lijian ametoa ufafanuzi pia kuhusu kikao cha karibuni cha viongozi wa Marekani, India, Japan na Australia, kilichokuwa na lengo la kuzuia ustawi na ushawishi wa kikanda na kimataifa wa China na akasema: Vita Baridi vimemalizika kitambo; na hakuna muungano wa aina yoyote wa kuidhibiti China utakaokubaliwa na kuweza kufika popote; zinachopaswa kufanya nchi hizo ni kuachana na fikra zilizopitwa na wakati za enzi za Vita Baridi na mtazamo usio sahihi wa kueneza mitazamo ya makabilianao ya kimakundi na mchezo wa kijiopolitiki; na badala yake zitoe mchango chanya wa kuleta amani na uthabiti katika eneo la Asia na Oceania.../