Russia: Hatutaki vita barani Ulaya wala Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80408-russia_hatutaki_vita_barani_ulaya_wala_ukraine
Rais wa Russia amesema kuwa nchi yake haitaki kutokee vita barani Ulaya wala nchini Ukraine na ni kwa sababu hiyo ndio maana imetoa pendekezo la kudhaminiwa usalama wa eneo hilo.
(last modified 2025-10-28T17:58:14+00:00 )
Feb 16, 2022 07:10 UTC
  • Russia: Hatutaki vita barani Ulaya wala Ukraine

Rais wa Russia amesema kuwa nchi yake haitaki kutokee vita barani Ulaya wala nchini Ukraine na ni kwa sababu hiyo ndio maana imetoa pendekezo la kudhaminiwa usalama wa eneo hilo.

Rais Vladimir Putin alisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari alipozungumza nao akiwa pamoja na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz mjini Moscow na kusisitiza kuwa, nchi za Magharibi zinapaswa kuacha kurundika silaha zao karibu na mpaka wa Russia na pia Jeshi la Nchi za Magharibi NATO liache kujizatiti kijeshi mashariki mwa Ulaya. 

Mgogoro katika uhusiano wa Russia na nchi za Magharibi hasa Marekani umekuwa mkubwa sana katika wiki za hivi karibuni hasa baada ya baadhi ya viongozi wa nchi za Ulaya na Marekani kudai kuwa Russia ina nia ya kuivamia kijeshi Ukraine. 

Russia inakanusha madai ya nchi za Magharibi kuwa inataka kuivamia kijeshi Ukraine na wakati huo huo lakini inasema kuwa haiwezi kufumbia macho maslahi yake ya kitaifa na inastahabu kutumika masuala ya kiufundi katika kadhia hiyo.

Madola ya Magharibi hasa Marekani yanachochea vita mashariki mwa Ulaya

 

Moja ya mambo yanayotakiwa na Moscow ni ahadi kutoka kwa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO kwamba kamwe haitoifanya Ukraine kuwa mwanachama wa jeshi hilo na pia nchi za Magharibi ziondoe wanajeshi wao mashariki mwa Ulaya kama ambavyo nchi hizo haziruhusu dola lolote kuwa na wanajeshi karibu na mipaka ya nchi hizo za Magharibi.

Nchi za Magharibi zinaitaka Russia iondoe wanajeshi wake kwenye mpaka wake na Ukraine suala ambalo linaishangaza Moscow na kusema kuwa, kuweko wanajeshi wake mpakani ni jambo la kawaida na ni haki ya kila nchi kuwa na wanajeshi wa mpakani. Russia inasema, lengo la Marekani na nchi za Magharibi ni kuzusha hali ya wasiwasi tu katika eneo hilo.