Jibu la China kwa tuhuma za Blinken
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin ameyataja matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken kuhusu mkoa wa Xinjiang kuwa ni shutuma zisizo na msingi. Katika ujumbe wake wa video, Blinken aliishutumu China kwa kuendeleza kile alichodai kuwa ni mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu katika mkoa wa Xinjiang.
Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imetumia kadhia kama vile Taiwan, hali ya haki za binadamu huko Hong Kong na hivi karibuni huko Xinjiang, ili kuongeza mashinikizo kwa serikali ya China na kujaribu kuishurutisha Beijing ifuate sera za Washington.
Kwa mtazamo wa duru mbalimbali za China, Marekani inaituhumu China kwa kukiuka haki za binadamu nchini humo, huku Marekani yenye ikiwa ni mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu, ndani na nje ya nchi hiyo.
Hata hivyo, kila mara Wademokrat wanapoingia madarakani nchini Marekani, huwa wanatumia haki za binadamu kama chombo cha mashinikizo dhidi ya wapinzani au washindani wa Marekani. Mbinu hii ya Washington sasa imechakaa katika uga wa kimataifa.
Hivi sasa utawala wa Wademokrt wa Rais wa Marekani Joe Biden unaibua kelele nyingi kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu nchini China.
Nozar Shafiei, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema hivi kuhusu kadhia hii:
Katika miaka ya hivi karibuni China imekuwa ikichapisha ripoti kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani, jambo linaloonyesha kuwa mzozo wa Beijing na Washington umeingia kwenye mvutano katika masuala ya haki za binadamu ambapo Marekani imekuwa ikionyesha kiburi na ubabe mkubwa katika kadhia hii.
Kilichopelekea kuongozeka shutuma za Marekani dhidi ya China katika siku za hivi karibuni ni suala la mgogoro wa Ukraine. Ukweli ni kwamba Marekani ina wasiwasi juu ya kuimarika ushirikiano na uhusiano baina ya China na Russia na hivyo kwa kutumia tuhuma za haki za binadamu inataka kuishinikiza Beijing iache kuinga mkono Moscow.
Marekani ina wasi wasi kuwa muungano mpya wa Mashariki katika karne ya 21 utapalekea kupungua satwa yake ya kibebebru na kuimarika nafasi ya bara Asia.
Abolfazl Zohrehvand, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusiana na hili:
Marekani inajua kwamba karne ya 21 ni karne ya bara Asia, na uchumi wa dunia utaegemeza zaidi upande huu wa mashariki mwa dunia.
Marekani inaamini kuwa China ndiyo chanzo cha hali hii ya kustawi kwa kasi kiuchumi bara Asia.
Kwa msingi huo, Marekani inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa satwa yake ya kibeberu duniani haisambaratiki. Washington ina wasiwasi kuhusu kuibuka madola mapya yenye nguvu yatakayobadlisha muelekeo wa mfumo wa kimataifa ambao Marekani inadai kuuongoza.
Pamoja na kuwepo wasiwasi huo wa Marekani, katika miaka ya hivi karibuni, China imejitahidi kuendeleza sera na mipango yake ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha mchakato wa ujenzi na ustawi katika Mkoa wa Xinjiang na kuufanya kuwa nguzo kuu ya mradi wa barabara mpya ya kimataifa kupitia Pakistan.
Marekani imekuwa ikitoa madai kuhusu utendaji wa serikali ya China katika mkoa wa Xinjiang ili kwa njia hiyo kuvuruga mradi mkubwa wa kiuchumi na usafiri wa Ukanda mmoja , Barabara Moja" ambao utaunganisha mabara ya Asia, Afrika na Ulaya.
China inatekeleza ajenda yake ya kiuchumi bila kujali madai na tuhuma zisizo na msingi za Marekani jambo ambalo limeikasirisha zaidi Washington.