Lavrov awashutumu Wamagharibi kwa kutoshughuliswa na wananchi wa Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amezishutumu Marekani na Umoja wa Ulaya kwa kutoshughulishwa na wananchi wa Ukraine na wala mambo yaliyopelekea kutokea vita nchini humo.
Sergeĭ Viktorovich Lavrov alisema hayo jana Jumatano katika hotuba yake kwenye Taasisi ya Kiserikali ya Uhusiano wa Kimataifa mjini Moscow na kuongeza kuwa, nchi za Magharibi ndizo zilizoanzisha vita vya Ukraine tarehe 24 Februari kwani zilichochea mambo chungu nzima na kudharau mambo mengine mengi ambayo ndiyo yaliyopelekea kuanza vita hivyo.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Russia amejibu pia ombi la wiki iliyopita la Poland la kutaka kutumwa askari wa kimataifa wa kulinda amani nchini Ukraine wakiwa na zana za kivita na kusisita kuwa, hatua hiyo inaweza kuiingiza kwenye vita vya ana kwa ana Russia na Jeshi la Nchi za Magharibi NATO.
Amesema pia kuwa, viongozi wa Ukraine wamelegeza misimamo yao katika mazungumzo na hatua hiyo itarahisisha kufikiwa makubaliano baina ya pande mbili.
Kabla ya hapo pia, Lavrov alikuwa ameishutumu vikali Marekani kwa siasa zake kuhusu vita vya Ukraine na kusema kuwa, Washington ndiyo inayokwamisha kufikiwa makubaliano baina ya Moscow na Kyiv hata katika masuala madogo kabisa.
Shutuma hizo za Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia dhidi ya Washington zimetolewa katika hali ambayo Marekani inajionesha kidhahiri kuwa ina hamu ya kufikiwa makubaliano ya kukomeshwa vita huko Ukraine huku wachambuzi wa mambo wakisema, Marekani inataka vita vya Russia na Ukraine viendelee ili nchi zote hizo mbili zidhoofike kijeshi na kiuchumi.