UNHCR: Wakimbizi 2,500 wamezama mwaka huu wakielekea Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i8191-unhcr_wakimbizi_2_500_wamezama_mwaka_huu_wakielekea_ulaya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetangaza kuwa wakimbizi wasiopungua 2,500 wamefariki dunia mwaka huu wakiwa katika safari ya hatari ya kuelekea barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 31, 2016 11:03 UTC
  • UNHCR: Wakimbizi 2,500 wamezama mwaka huu wakielekea Ulaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetangaza kuwa wakimbizi wasiopungua 2,500 wamefariki dunia mwaka huu wakiwa katika safari ya hatari ya kuelekea barani Ulaya.

Taarifa ya UNHCR imetolewa huku shirika hilo la Umoja wa Mataifa likieleza wasiwasi uliopo wa wakimbizi wengine wengi kufikwa na hatima hiyo hiyo.

Kwa mujibu wa UNHCR idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na muda kama huo katika mwaka uliopita wa 2015 ambapo wakimbizi wapatao 1,855 walizama baharini.

Msemaji wa UNHCR William Spindler, amesema hali hiyo inathibitisha kwamba mwaka huu wa 2016 ni mwaka hatari zaidi kwa maafa ya wakimbizi. Aidha amesisitizia umuhimu wa kutekelezwa operesheni za uokoaji kama hatua mojawapo ya kufuatilia nyendo za wakimbizi na wahamiaji katika bahari ya Mediterania na vile vile haja ya kuchukuliwa hatua mbadala za uhakika na salama zaidi kwa ajili ya watu wanaohitaji hifadhi ya kimataifa.

Tamko la Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limekuja kufuatia wiki ya maafa makubwa zaidi kutokea katika mwaka huu wa 2016 ya vifo vya wakimbizi baada ya watu wasiopungua 880 kufariki dunia wakati vyombo vya majini vilivyowabeba vilipozama katika pwani za Libya na Italia.

Tangu ulipoanza mwaka huu, watu wasiopungua 203,981 wamefanya safari za baharini kuelekea Ulaya, ambayo ni idadi sawa na wale walioweza kuwasili barani humo katika kipindi kama hiki mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kushughulikia Wahamiaji (IOM) wakimbizi wengi waliosafiri kuelekea Italia wanatoka Nigeria, Gambia, Senegal, Guinea na Ivory Coast.../