Mar 30, 2022 11:48 UTC
  • Waislamu India wakasirishwa na uamuzi wa mahakama ulioidhinisha matamshi ya chuki

Wimbi la kejeli na hasira limetanda katika mitandao ya kijamii nchini India baada ya mahakama kufunga kesi dhidi ya wanasiasa wawili waliotoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Waislamu, ikisema kuwa uchochezi si kauli za chuki ukiambatana na tabasamu.

Suala hilo linahusiana na uchaguzi wa India huko New Delhi mnamo 2020, wakati wanasiasa wawili wa chama tawala cha Wahindu cha Bharatiya Janata Party (BJP), Anurag Thakur na Parvesh Verma walipochochea matumizi ya nguvu dhidi ya Waislamu, wakiwataja kuwa ni "wavamizi wanaovunja nyumba, kubaka wanawake na kuua watu", kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya India.

Baada ya hapo kiongozi wa Chama cha Kisoshalisti cha India, Brenda Karat, akifuatana na mwanasiasa wa India KM Tiwari, waliwasilisha kesi dhidi ya Thakur na Verma, kwa madai ya kueneza chuki na uhasama dhidi ya Waislamu na waandamanaji. 

Uamuzi wa kesi hiyo ulitolewa na Mahakama Kuu ya Delhi Ijumaa iliyopita, huku jaji wa mahakama hiyo akisema, kama matamshi hayo ya uchochezi yaliambatana na tabasamu hayawezi kutambuliwa kuwa ni uchochezi!

"Ukisema jambo kwa tabasamu, sio kosa, na ukisema jambo la kuudhi kwa hasira, wewe ni mtenda dhambi, tunapaswa kuangalia muktadha", amesema jaji wa Mahakama Kuu ya Delhi kuhusu matamshi yaliyotolewa na wanasiasa hao wawili wakiwahimiza wafuasi wa chama tawala kuwaua Waislamu.

Wanaharakati kwenye mitandao ya kijamii wamekosoa na kukejeli uamuzi huo, wakiutaja kuwa unakipendelea chama tawala cha Wahindu. 

Mwanasiasa wa India, Panthan Khan ameweka kwenye akaunti yake ya Twitter picha ya mhalifu katika chumba cha mahakama, akiwa na kisu chenye damu mkononi mwake huku akisema, "Nimemuua nikitabasamu," akiashiria uamuzi wa mahakama ya Delhi.

Chuki na hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeshika kasi sana nchini India katika miezi ya karibuni. 

Hivi karibuni Mahakama ya Juu ya jimbo la Kusini mwa India la Karnataka iliidhinisha marufuku ya vazi la Hijabu katika shule na vyuo vikuu vya jimbo hilo. 

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa marufuku ya vazi la hijabu inakiuka wajibu wa India chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, ambayo inadhamini haki ya uhuru wa imani ya kidini ya mtu binafsi na uhuru wa kujieleza na kupata elimu bila ubaguzi.

Tags