Mar 31, 2022 02:27 UTC
  • Stéphane Dujarric
    Stéphane Dujarric

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema miito ya kutaka Russia iondolewe kwenye Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo ni hatari na inazusha wasiwasi.

Maseneta wanane wa chama cha Democrat na wanne kutoka chama cha Republican nchini Marekani siku ya Jumanne walimwandikia barua balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield, wakiashiria hatua ya Russia ya kuishambulia kijeshi Ukraine na kumtaka balozi huyo awasilishe azimio la kutaka Russia iondolewe katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Kuiunga mkono Ukraine ni moja ya masuala vinavyoafikiana kwa kauli moja vyama vyote viwili vya siasa nchini Marekani, na hadi sasa vimeshaidhinisha misaada ya fedha kwa ajili ya serikali ya nchi hiyo.

Tarehe 24 Februari na kufuatia msimamo wa Magharibi wa kupuuza wasiwasi wa kiusalama wa Russia, nchi hiyo ilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Ukraine kwa lengo la kuipokonya silaha nchi hiyo.

Jana Jumatano, Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema, mwito huo ni ombi lililotolewa na nchi wanachama ambazo ndizo zilizotunga sheria na kuasisi chombo hicho cha Baraza la Haki za Binadamu.

Lakini Dujarric akaongezea kwa kusema: "kama nilivyotangulia kueleza awali kuhusu Shirika la Kimataifa la Utalii, narudia kusema tena kuwa suala kama hili ni hatari na litazusha wasiwasi."

Baraza la utendaji la Shirika la Kimataifa la Utalii, mnamo tarehe 8 Machi lilifanya kikao chake cha kwanza mjini Madrid, Uhispania kujadili pendekezo la kusimamisha uanachama wa Russia ambalo limewasilishwa kwa pamoja na Guatemala, Lithuania, Poland, Slovania na Ukraine.../

 

Tags