Sisitizo la China la kuzidishwa ushirikiano kati yake na Russia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema ushirikiano wa nchi yake na Russia hauna mpaka. Wang Wenbin amesisitiza kuwa ipo haja ya kuendelezwa ushirikiano kati ya China na Russia katika sekta mbalimbali ikiwemo masuala ya usalama.
Matamshi hayo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China kuhusu kuendeleza ushirikiano na Russia ambayo yamekuwa yakisikika mara kwa mara kutoka kwa viongozi wengine wa Beijing, ni jibu kwa mashinikizo ya kiuchumi, kijeshi na kiusalama ya nchi za Magharibi hasa Marekani dhidi ya Russia. Nchi hiyo imekumbwa na mashinikizo makubwa ya nchi za Magharibi katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika sekta za biashara, uchumi, benki na usalama baada ya kuishambulia Ukraine Februari 24 mwaka huu. Marekani na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) ambazo zimekuwa na nafasi kuu katika kuchochea vita vya Ukraine, zinadai kuwa zinaiunga mkono Kyiv mkabala wa Moscow kupitia hatua zao za kuzidisha vikwazo kwa Russia. Kidhahiri inaonekana kuwa, Marekani imefanikiwa kutengeneza mazingira ya kikanda ya kuzidisha mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Russia. Wakati huo huo, China, ambayo imepanua uhusiano wake na Russia katika miaka ya hivi karibuni, inajaribu kuimarisha msimamo wake dhidi ya Marekani ikiwa bega kwa bega na Moscow.
Ali Akbar Jokar, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anazungumzia hilo akisema: Uhusiano wa China na Russia katika muongo mmoja wa karibuni umestawi pakubwa na sasa ambapo Russia imewekewa vikwazo na nchi za Magharibi, Moscow inataraji kuungwa mkono zaidi na China, ajambo ambalo limeathiriwa zaidi na hali inayoshuhudiwahivi sasa.
Weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa, lengo kuu la Marekani kuchochea vita kati ya Russia na Ukraine ni kuzusha mtengano baina ya Beijing na Moscow. Hii ni kwa sababu, kwa mtazamo wa Magharibi, muungano utakaoibuka kati ya China na Russia unaweza kuhatarisha nafasi ya Marekani duniani; na wakati huohuo kuzuia udhibiti wa nchi za Magharibi. Kwa msingi huo, kadiri mahasimu wa Marekani watakavyozidi kuwa karibu zaidi au kuimarisha nafasi na ushawishi wao katika masuala ya kimataifa, ndivyo Magharibi pia inavyozidi kuwa na wasiwasi kuhusu kupungua nguvu zake.
Zbigniew Brzeziński aliyekuwa Mshauri wa Usalama wa Taifa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter anasema kuhusu hilo kwamba: "Ili kudumisha udhibiti wa kimataifa wa Marekani kuna ulazima wa kuyadhibiti madola ya Eurasia. Hii ni kwa sababu, eneo hilo ni sehemu ya awali ambako madola ya Eurasia yanataka kuwa ushawishi ili kuzidisha nguvu yao kimataifa. Kwa hiyo, Marekani kwanza inapasa kuibua mizozo ili kuzidhoofisha Russia na China na hivyo kuyumbisha amani katika maeneo yao.
Alaa kull hal, hatua ya China ya kutilia mkazo suala la kupanua zaidi uhusiano wake na Russia bila ya mipaka inaweza kuwa jambo jambo zuri lenye kuipa moyo Moscow ambayo inaendelea kukumbwa na mashinikizo ya vikwazo vya Marekani na washirika wake. Pamoja na hayo, kinachotawala mahusiano ya kimataifa ni kila nchi kupigania maslahi yake ya taifa katika kila uhusiano wa kisiasa na kiuchumi. Ukweli ambao bila shaka unatawala pia katika uhusiano kati ya Beijing na Moscow.