Waziri Mkuu wa Pakistan asema, Marekani inapanga njama ya kumuondoa madarakani
-
Imran Khan
Waziri Mkuu wa Pakistani, Imran Khan amedokeza kuwa huenda akakataa matokeo ya kura ya kumuondoa madarakani akieleza kuwa kura hiyo ni njama iliyoratibiwa na Marekani ambayo ameituhumu kwa kujaribu kupindua utawala wake.
Ni baada ya wabunge wa upinzani nchini Pakistan kuwasilisha pendekezo la kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Imran Khan bungeni, wakitumai kuiondoa madarakani serikali yake huku kukiwa na shutuma kwamba amesimamia vibaya uchumi wa taifa hilo.
Imran Khan amewaambia waandishi habari wa kigeni kwamba anawezaje kukubali matokeo na kura za wabunge wakati mchakato mzima umepuuzwa? Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kuwa, harakati za kutaka kumuondoa madarakani ni uingiliaji wa wazi wa Marekani katika siasa za ndani za Pakistan na kwamba ni jaribio la "kubadilisha utawala."
Khan, ambaye alipoteza wingi wa viti vya Bunge baada ya washirika wake wakuu kujiondoa katika serikali yake ya mseto na kujiunga na upinzani, ametoa wito kwa wafuasi wake kufanya maandamano leo Jumapili kabla ya kupigwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Kiongozi wa upinzani katika Bunge la Kitaifa la Pakistan, Shehbaz Sharif, alipendekeza hoja ya kutokuwa na imani dhidi ya Khan siku ya Jumatatu iliyopita.

Imran Khan anaamini kuwa mashinikizo ya vyama vya upinzani yanayomtaka ajiuzulu yanatokana na njama za nchi za kigeni kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali yake kutokana msimamo wake usioyumba kuhusu siasa zake za nje na ndani ya nchi.
Khan, 69, nahodha wa zamani wa timu ya kitaifa ya kriketi ya Pakistan, aliingia madarakani katika uchaguzi wa 2018, na kupata kura 176. Anahitaji kura 172 ili kusalia madarakani.