Iran yaitaka Marekani kuchukua hatua zaidi juu ya makubaliano ya nyuklia
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Marekani kuchukua hatua zaidi katika kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna, kati ya Tehran na kundi la 5+1.
Katika kikao na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Finland Timo Soini mjini Helsinki jana Jumanne, Mohammad Javad Zarif alisema ingawa Marekani imeandaa mazingira ya kuona kuwa benki za dunia hazitowekewa vikwazo kwa kushirikiana na benki za humu nchini, lakini anaamini kuwa serikali ya Washington inaweza kuchukua hatua zaidi katika kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu inafufua biashara na nchi hizo kikamilifu, ikiwa ni katika utekelezaji wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Ameongeza kuwa, nchi nyingi kama vile Japan, Korea Kusini, nchi za bara Asia na Ulaya zimesaini makubaliano ya kuhuisha ushirikiano wa kibiashara na kibenki na Iran lakini baadhi ya benki za Ulaya zingali zinasita kufufua uhusiano wao wa kibenki na Tehran zikihofiwa kutengwa na Marekani.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland amesema Helsinki na Tehran zimekuwa na ushirikiano mwema kwa muda mrefu na haswa katika nyuga za elimu na mawasiliano. Ameelezea umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbali wakati huu ambapo Iran imeondolewa vikwazo.
Aidha jana Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif alifanya mazungumzo na Rais wa Finland, Sauli Niinisto na kubadilishana mawazo juu ya hatua za kuchukuliwa ili kuboresha mahusiano ya pande mbili katika nyuga tofauti, mbali na suala la kutatuliwa migogoro katika nchi za magharibi mwa bara Asia.