Taathira hasi ya vita vya Ukraine juu ya uchumi wa dunia
Ikiwa zimepita siku 47 tangu kuanza vita vya Russia na Ukraine, hasara za kiuchumi za vita hivyo zinaongezeka siku baada ya nyingine, kadiri kwamba Shirika la Biashara Duniani WTO limetangaza katika ripoti yake ya karibuni kwamba vita hivyo vimeathiri vibaya uchumi wa dunia.
Shirika hilo la kimataifa linatabiri kuwa ukuaji wa biashara duniani utapunguka kwa nusu mwaka huu na kwamba ukuaji wa pato jumla la taifa kimataifa utapungua kwa kiasi kikubwa.
Shirika la Biashara Duniani linatabiri kwamba mgogoro uliosababishwa na vita vya Russia na Ukraine unaweza kupunguza ukuaji wa pato hilo kwa asilimia 0.7 hadi 1.3.
Utafiti unaonyesha kuwa vita vya Russia na Ukraine vimeathiri sana uchumi wa nchi hizo mbili hizo kiasi kwamba sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo ya Ukraine haijalimwa na uharibifu wa vita na ukosefu wa usalama umefanya hali ya uchumi kuwa ngumu nchini humo.
Loulia Sviridenko, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Uchumi wa Ukraine anaashiria taathira zisizo za moja kwa moja za vita kwa uchumi wa nchi hiyo, zikiwemo za mlipuko wa ukosefu wa ajira, kupungua pakubwa matumizi ya bidhaa katika familia na kupungua pato la serikali na kusema: "Hasara kubwa inaonekana kwenye sekta ya miundombinu ambapo takriban kilomita 8,000 za barabara zimeathirika au kuharibiwa kabisa, na makumi ya vituo na viwanja vya ndege vyenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 108 kupata hasara.
Hii ni katika hali ambayo vita hiyo vya Ukraine pia vimekuwa na taathira kubwa hasi kwa uchumi wa dunia. Russia na Ukraine ni wauzaji wakuu wa bidhaa za kimkakati duniani na zina nafasi muhimu katika usambazaji wa nafaka, chakula na nishati duniani. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, chakula cha zaidi ya nusu ya watu wenye njaa duniani mwaka 2021 kilitoka Ukraine. Russia pia ni mzalishaji mkuu wa virutubisho vya udongo kama vile potashi na fosfeti, ambazo ni sehemu muhimu ya uzalishaji wa mbolea za kemikali. Kwa hivyo, sekta ya kilimo sasa imeathirika kote ulimwenguni.
Aidha, ukosefu wa usalama na kutengwa sehemu kubwa ya bajeti kwa ajili ya masuala ya usalama na silaha kumepunguza ukuaji wa uchumi na kuzidisha matatizo katika pembe zote za dunia.
Lawrence Boone, mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo anasema: "Vita vya Ukraine vinaathiri kiwango cha ukuaji wa uchumi barani Ulaya na vinatarajiwa kuongeza mfumuko wa bei kwa nukta mbili hadi mbili na nusu."
Hili hiyo pia imeathiri uchumi wa Marekani.
Cecilia Rouse, mwenyekiti wa baraza la ushauri wa kiuchumi la serikali ya Biden anasema: "Operesheni ya Russia nchini Ukraine imeleta changamoto zaidi za kiuchumi na kuibua mfumuko wa bei nchini Marekani." Bei ya petroli wakati huo huo, imeongezeka hadi zaidi ya dola 4 kwa galoni moja, kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka 14 iliyopita. Takwimu za hivi karibuni pia zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei nchini Marekani umefikia karibu asilimia 8.
Gerry Rice, Msemaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) amesema kupanda kwa bei ya mafuta duniani kumeathiri pakubwa biashara ya kimataifa na kuzishtua chumi ndogo.
Kutokana na kutofahamika vyema hatima ya vita vya Ukraine, wasiwasi wa kuendelea vita hivyo kwa muda mrefu umeongezeka kwani vinaweza kupelekea njaa na umaskini kuongezeka duniani hasa katika nchi dhaifu.
Kuhusu kadhia hiyo Bita Yavrchik, mwanauchumi mkuu katika Benki ya Maendeleo ya Ulaya anasema: “Matatizo ya nishati, kilimo, mfumuko wa bei, umaskini na kadhalika yote hayo yanaashiria kwamba vita vya Ukraine vitakuwa na madhara makubwa duniani, ikiwa ni pamoja na kudorora kwa ukuaji wa uchumi.”