Wademokrati wataka kuangaliwa upya uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia
(last modified Thu, 14 Apr 2022 07:54:12 GMT )
Apr 14, 2022 07:54 UTC
  • Wademokrati wataka kuangaliwa upya uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia

Wademokrati wa Kongresi ya Marekani wanasema, kuiunga mkono Saudi Arabia ni "kinyume" na maslahi ya Marekani.

Jarida la Wall Street limeripoti kuwa, viongozi wa Kamati za Bunge za Mambo ya Nje na Ujasusi, na zaidi ya Wademokrati wengine 20 wanapanga kuishinikiza serikali ya Rais Joe Biden ichukue msimamo mkali zaidi dhidi ya Saudi Arabia, na katika uwanja huo wanaashiria hatua ya Riyadh ya kukataa kushirikiana na Washington katika suala la mashambulizi ya Russia huko Ukraine na masuala kadhaa ya haki za binadamu.

Wabunge hao wameandika katika barua yao kwamba: "Tuko katika hatua ya mabadiliko: Marekani inaweza kuendelea kumunga mkono mshirika mwenye mwenye utawala wa kiimla, au tunaweza kupanga upya uhusiano wetu katika kutetea haki za binadamu."

Wabunge hao pia wamebainisha kuwa, Saudi Arabia imekataa ombi la Marekani la kuzidisha uzalishaji wa mafuta ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo iliyopanda kutokana na vita vya Ukraine, na imeingia katika mazungumzo na Beijing kuhusu uuzaji wa mafuta yake kwa China kwa kutumia sarafu ya Yuan.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2020, Joe Biden aliitaja Saudi Arabia kama nchi isiyotakikana na aliahidi kuiwajibisha serikali ya Saudia kwa ukiukaji wa haki za binadamu; lakini hadi sasa hajachukua hatua za maana katika uwanja huo. 

Tags