China yaonya kuhusu matokeo mabaya kimataifa ya vikwazo dhidi ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i82524-china_yaonya_kuhusu_matokeo_mabaya_kimataifa_ya_vikwazo_dhidi_ya_russia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameonya dhidi ya kuenea ulimwenguni taathira hasi za vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia. Zhao Lijian pia ameitaka Marekani kuchukua jukumu maalum la kuzingatia sheria za mfumo wa uchumi wa dunia na kudumisha uthabiti wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2022 03:03 UTC
  • China yaonya kuhusu matokeo mabaya kimataifa ya vikwazo dhidi ya Russia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameonya dhidi ya kuenea ulimwenguni taathira hasi za vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia. Zhao Lijian pia ameitaka Marekani kuchukua jukumu maalum la kuzingatia sheria za mfumo wa uchumi wa dunia na kudumisha uthabiti wake.

Siasa za Marekani kuhusiana na mgogoro wa Ukrain daima zimekuwa zikikosolewa kimataifa ikiwemo China. Washington inafanya juhudi za kuzilazimisha nchi nyingine za dunia zifuate siasa zake hizo kuhusiana na mgogo huo na inatumia kila wenzo ukiwemo wa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi yoyote inayopinga na kukataa kufuata siasa hizo za mabavu.

Mbali na hayo, Marekani imekuwa ikiwashinikiza washirika wake kwa ajili ya kutekeleza vikwazo mbalimbali dhidi ya Russia na nchi kama vile Australia, ili ipate kuimarisha nafasi yake katika mfumo wa siasa za kieneo za Marekani, imekuwa ikiongeza vikwazo dhidi ya Russia ambapo hatua ya karibuni kabisa iliyochukuliwa na nchi hiyo dhidi ya Russia ni kuyawekea vikwazo mashirika yake 14.

Zhao Lijian

Tukiachilia mbali aina ya uhusiano uliopo kati ya Russia na nchi kama vile Australia ambao unaifanya daima itake kuongeza mashinikizo dhidi ya Moscow kupitia vikwazo, suala lililo na umuhimu katika mtazamo wa duru za kimataifa ni kuwa jambo hilo ambalo linatokana na fikra na uchochezi wa vita baridi wa Marekani, linaweza kuwa na taathira nyingi hasi kwa uchumi wa dunia.

Gary Hoffeuer, mchambuzi wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu kadhia hiyo kwamba licha ya hatua zote ambazo zimechukuliwa na Marekani na washirika wake wa Ulaya dhidi ya Russia ili isimamishe mashambulizi yake huko Ukraine lakini hatua hizo hazijakuwa na natija yoyote ya maana hadi sasa bali unaoumia ni uchumi wa dunia.

Wataalamu wengi wa mambo wanaamini kuwa kwa kutumia kisingizio cha mgogoro wa Ukraine, Marekani inajaribu kuzuia kuongezeka nguvu ya Muungano wa Mashariki kati ya China na Russia na vile vile nchi nyingine za eneo na inatumia kile inachoona kuwa ni nguvu yake ya kimataifa kujaribu kuzima au kupunguza kasi ya kuimarika nguvu ya Moscow na Beijing.

Kuibuia mgawanyiko kati ya nchi za Mashariki na washirika wa Russia sambamba na kuyashinikiza mataifa mengine yafuate siasa za Marekani dhidi ya Moscow ni miongoni mwa malengo makuu yanayofuatiliwa na White House kwa kuendelea kupiga ngoma ya vita huko Ukraine. Hii ni katika hali ambayo hata Wamarekani wenyewe wanakiri kwamba nchi hiyo imeshindwa kufikia malengo hayo.

Ngano ni miongoni mwa mazao muhimu ya kilimo ambayo yameathirika na vita vya Ukraine

 

Michael Zovaeec, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia kimsingi ni vya kimaonyesho tu na hiyo ndio maana hadi sasa havijakuwa na taathira yoyote katika kuabdilisha mienendo ya Russia kuhusu mgogoro wa Ukraine, na Vladimir Putin na Sergey Lavrov, Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia kwa utaratibu huo wana kinga dhidi ya vikwazo hivyo.

Kwa vyo vyote vile na kwa mtazamo wa duru za Magharibi, China pia ina nafasi yake muhimu ambayo inaitekeleza katika mogoro wa Ukraine. Kwa maana kwamba ikiwa ni nchi huru isiyoegemea upande wowote, China inakosoa siasa za Marekani kuhusu vita vya Ukraine na kwa kukariri matokeo mabaya ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia kwa uchumi wa kimataifa, inakusudia kuibua mgawanyiko kati ya nchi za Magharibi. Hata hivyo baadhi ya duru huko Magharibi zinaamini kuwa matamshi yanayotolewa na viongozi wa China kuhusu taathira hasi za vikwazo vya nchi hizo dhidi ya Russia kwa uchumi wa dunia, ni nara tupu na kwamba China yenyewe inafuatilia malengo yake binafsi katika mgogoro huo.