Apr 26, 2022 13:26 UTC
  • Kuendelea mvutano baina ya Marekani na mataifa ya mrengo wa kushoto ya Amerika ya Latini

Marekani ingali inaendeleza siasa zake za chuki na hasama dhidi ya mataifa ya mrengo wa kushoto ya Amerika ya Latini.

Katika uwanja huo, Cuba ikiwa moja ya mataifa muhimu katika eneo la Amerika ya Latini, haijaalikwa katika mkutano wa wakuu wa Bara la Amerika uliopangwa kufanyika Juni mwaka huu. Bruno Rodriguez, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba sanjari na kulaani hatua ya Washington ya kuifuta nchi yake katika mkutano huo ujao amesema, lengo la kutoalikwa Cuba katika mkutano huo lina matamashi ya kisiasa na kwamba, hatua hiyo ni sehemu ya vigezo vya kindumakuwili ambavyo vinahusiana na hali ya ndani na ya uchaguzi nchini Marekani.

Kwa miaka mingi sasa Marekani imekuwa ikifanya njama za kuwa na ushawishi katika eneo la Amerika ya Latini na kuziingiza madarakani tawala ambazo ni vibaraka wake hususan katika mataifa ya mrengo wa kushoto kama Venezuela, Bolivia, Cuba na Nicaragua. Licha ya vitisho na kutekeleza siasa za hasama na chuki, lakini hadi sasa Washington imeshindwa kufikia malengo yake ya kuyafanya mataifa hayo yawe na utii kwake.

cubaBaadhi ya mataifa ya Amerika ya Latini kwa kuzingatia tajiriba ya kihistoria na kupitia kipindi cha kuwa tegemezi kwa Marekani, ni kwa miongo kadhaa sasa ambapo yamekuwa yakizipa kipaumbele sera za kupigania uadilifu na zilizo dhidi ya ukoloni na wakati huo huo kutetea uhuru.

Kama alivyosisitiza Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba ni kwamba, Marekani inapaswa kudiriki kwamba, eneo la Amerika ya Latini limebadilika milele na hakuna nafasi tena katika eneo hilo ya kutwishwa au kupenyeza mitazamo ya Washington.

Hata hivyo licha ya muqawama na kusimama kidete mataifa ya Amerika ya Latini, lakini viongozi wa Marekani hawajakataa tamaa na wamekuwa wakitumia aina kwa aina ya nyenzo ili kuyafanya mataifa ya eneo hilo yasalimu amri. Viongozi wa Marekani wakitumia visingizo kama vya kutetea haki za binadamu na demokrasia wamekuwa wakikataa kuutambua ushindi wa vyama vya mrengo wa kushonto uliopatikana kwa njia ya uchaguzi huru na wa haki. Ili kufikia malengo yao, viongozi wa Marekani wamekuwa wakizitumia hata asasi za kieneo. Hilo linashuhudiwa wazi ambapo Jumuiya ya Mataifa ya Amerika imegeuka na kuwa wenzo wa Washington wa kuyashinikiza mataifa ya eneo hilo.

Kuhusiana na hilo, wiki iliyopita, Baraza Kuu la Jumuiya ya Mataifa ya Amerika lilipasisha azimio ambalo lilitangaza wazi kwamba, uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini Nicaragua haukuwa wa haki, wazi na uadilifu na hivyo hauna uhalali wa kidemokrasia.

Msimamo huo ulikabiliwa na upinzani mkali wa serikali ya Nicaragua ambayo ilitangaza kwamba, itajitoa katika jumuiya hiyo. Kabla ya hapo pia, Venezuela imewahi kulalamikia utendaji wa kindumakuwili wa jumuiya hiyo na ikachukua uamuzi wa kujiondoa.

Pamoja na hayo yote, inaonekana kuwa, viongozi wa Marekanji wangali wanaota ndoto za alinacha za kutaka kulidhibiti na kulitawala eneo la Amerika ya Latini. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa, njama zote za Marekani zimefeli na hivyo, viongozi wa Washington hawana budi kukiri kwamba, mipango yao michafu imefeli na kugonga mwamba.

Hivi sasa hali ya mambo katika eneo hilo inaonyesha kwamba, haiendi kama inavyotaka Marekani na hivyo tunaweza kutabiri kwamba, njama za Washington za kuingilia mambo ya ndani ya mataifa hayo, zitachukua mkondo na wigo mpana zaidi katika siku za usoni.

Tags