'Janga la Kimaumbile' latangazwa Paris kufuatia mafuriko
Rais Francois Hollande wa Ufaransa ametangaza 'maafa ya kibinadamu' katika mji mkuu wa nchi hiyo kufuatia mvua kali ambazo zimesababisha mafuriko makubwa.
Maafisa mjini Paris wamefunga makavazi (jumba la makumbusho) maarufu duniani ya Louvre baada ya mto Seine kufuruka jana na kuzusha hofu ya kutokea tena janga la mafuriko kama la mwaka 1910. Kwa mujibu wa waziri wa mazingira wa Ufaransa Bi. Ségolène Royal, asilimia 50 ya miji ya Ufaransa iko katika hatari ya kuharibiwa na mafuriko, huku watu milioni 17 kati ya watu wote milioni 67 nchini humo wakiwa wanaishi katika maeneo ambayo yana hatari ya kuharibiwa na maji ya bahari, mito na mitano inayofurika. Tokea rekodi za mvua zianze kuandikwa mwaka 1873, hii ni mara ya kwanza kwa mji wa Paris kushuhudia kiasi hiki kikubwa cha mvua za mwezi Mei. Watu 25,000 mjini Paris hawana umeme na wengine 3,000 wamehamishwa kutoka mji wa Nemours kutokana na mafuriko. Ufaransa imekumbwa na mafuruko katika hali ambayo nchi hiyo katika siku za hivi karibuni imekuwa ikishuhudia machafuko, maandamano na migomo ya wafanyakazi wanaopinga sheria mpya ya leba ambayo wanasema ni ya kidhalimu. Eneo la Kaskazini mwa Ulaya limekumbwa na mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuruko katika nchi za Ubelgiji, Ujerumani na Ufaransa. Watu 11 wamepoteza maisha katika siku hivi karibuni kote barani Ulaya kutokana na mafuriko, wengi wao wamepoteza maisha nchini Ujerumani.