Jun 13, 2022 11:18 UTC
  • Kamati ya Bunge: Tuna ushahidi wa kumtia hatiani Trump

Wanachama wa Kamati ya Bunge la Marekani inayochunguza shambulio dhidi ya jengo la Kongresi tarehe 6 Januari mwaka jana, wamesema wana ushahidi wa kutosha wa kumtia hatiani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump.

Jopo hilo la uchunguzi limesema kuwa limekusanya ushahidi wa kutosha wa kumweka kwenye hatia Trump, kwa jaribio lake la kutaka kupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020.

Vikao vya kamati hiyo vya kupokea ushahidi kutoka kwa umma vilivyoanza wiki iliyopita vinakusudia kujenga kesi imara dhidi ya Trump, na kumbebesha dhima ya shambulio hilo, kwa kueneza uvumi juu ya uchaguzi, kujaribu kubadilisha matokeo na kuchochea pamoja na kuyakusanya magenge yaliyoshambulia Kongresi mnamo Januari 6.

Aidha Trump anaandamwa na shitaka la kufeli kuzuia ghasia na mashambulizi dhidi ya jengo la Kongresi lililofanywa na wafuasi wake wenye misimamo mikali.

Wafuasi wa Trump wenye misimamo mikali

Mapema mwaka huu, Trump alisema iwapo atagombea na kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2024, atawasamehe na kuagiza kuachiwa huru watenda jinai waliohusika na shambulizi dhidi ya jengo la Kongresi mnamo tarehe 6 Januari mwaka jana, lililofanywa na wafuasi wake.

Ikumbukwe kuwa, kikao cha Kongresi ya Marekani ambacho kilifanyika kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020 huko Marekani kilikabiliwa na shambulio la wafuasi wa Trump na kusimama kwa masaa kadhaa. Watu wasiopungua watano wakiwemo maafisa usalama wa nchi hiyo waliuawa katika shambulio hilo la kutisha, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. 

 

Tags