Jun 28, 2022 07:57 UTC
  • UNODC: Mamilioni ya vijana duniani wamezama katika uraibu wa mihadarati

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika na Jinai na Mihadarati (UNODC) imesema watu zaidi ya milioni 284 duniani wenye umri kati ya miaka 15 na 24, walitumia aina mbalimbali ya mihadarati mwaka juzi 2020, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 26 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Ofisi hiyo ya UN ilisema hayo jana Jumatatu katika ripoti yake iliyopewa anuani ya 'Ripoti ya Mihadarati Duniani 2022' na kuongeza kuwa, tabaka la vijana ndilo lililotumbukia zaidi katika mgogoro na uraibu wa mihadarati katika nchi mbalimbali duniani.

Ripoti hiyo imesema idadi ya watu wanaosumbulia na magonjwa tofauti kwa kutumia dawa za kulevya imeongezeka na kufikia watu milioni 38.6, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa, bangi ndiyo mihadarati inayotumiwa na watu wengi zaidi duniani, ambapo mwaka juzi 2020, watu milioni 209 walitumia dawa hiyo ya kulevya. Uraibu wa bangi umeongezeka hadi asilimia 26 ndani ya muongo mmoja uliopita.

Ripoti hiyo imesema hatua ya 'kuhalalishwa' matumizi ya bangi katika sehemu mbalimbali za dunia imechangia kuongezeka matumizi ya kila siku ya mihadarati hiyo, na taathira zake hasi za kiafya.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika na Jinai na Mihadarati (UNODC) imeeleza kuwa, karibu watu milioni 61 ni waraibu wa afyuni, milioni 34 wa mihadarati aina ya amphetamine, milioni 21 wanabugia cocaine, huku milioni 11 wakitumia mihadarati ya kujichoma kwa sindano.

Mwaka 2019, watu zaidi ya 494,000 walipoteza maisha kutokana na utumiaji wa mihadarati, huku watu 93,000 wakiaga dunia nchini Marekani baina ya mwaka 2019 na 2020, kutokana na matumizi ya afyuni na mifano yake.

 

Tags