Rais wa zamani wa Russia aonya kuhusu 'Siku ya Kiyama'
Rais wa zamani wa Russia ameionya vikali Ukraine na kusema kuwa, iwapo Kiev itathubutu kulishambulia eneo la Crimea, basi Kiyama kitawafikia wao pamoja na washirika wao kwa wakati mmoja.
Dmitry Medvedev ambaye ni Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia alitoa indhari hiyo jana Jumapili katika mkutano wake na Maveterani wa Vita vya Pili vya Dunia na kueleza kuwa, "....vikaragosi vinavyojaribu kututisha juu ya Crimea vinapaswa kutambua kuwa, kushambulia eneo hilo (Crimea) kutapelekea Siku ya Malipo kuwafikia wote hao."
Amezihutubu nchi za Magharibi kwa kusema, wanaoendelea kuchochea hali ya mambo na kutoa vitisho kupitia taarifa wanapaswa wajue kuwa, iwapo Crimea itashambulia na kisha Russia iamue kujibu mapigo, hali itakuwa mbaya hapatakuwa na pahala pa kujificha.
Amesema viongozi wa Ukraine watambue kuwa, hakuna shaka Russia itafikia malengo yake yote katika operesheni yake ya kijeshi, ikiwemo kusambaratisha jeshi la nchi hiyo ya Ulaya Mashariki, na kutokomeza Unazi.
Kisiwa cha Crimea mwaka 2014 kilitangaza kuwa huru na kujitenga kwa upande mmoja na Ukraine baada ya kufanyika kura ya maoni.
Kisiwa hicho kiliwasilisha ombi la kujiunga na Russia; ombi ambalo liliidhinishwa na Russia baada ya viongozi wa nchi hiyo kusaini makubaliano ya kujiunga kisiwa hicho na Russia.