Joto kali limeua watu 500 nchini Uhispania
(last modified Thu, 21 Jul 2022 04:19:35 GMT )
Jul 21, 2022 04:19 UTC
  • Joto kali limeua watu 500 nchini Uhispania

Waziri mkuu wa Uhispania amesema zaidi ya watu 500 wamepoteza maisha nchini humo wakati wa wimbi la joto la siku 10 huku bara lote la Ulaya likiendelea kupata hasara kubwa kutokana na joto kali ambalo limevunja rekodi mwaka huu.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema hali hivi sasa ni ya hatari na kuongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni ukweli ambao hauwezi kupingika huku akiwahimiza wananchi kuchukua tahadhari.
Sanchez amesema takwimu hizo za waliopoteza maisha zimewasilishwa na Taasisi ya Afya ya Carlos III ambayo inakadiria idadi ya vifo vinavyotokana na joto itaongezeka mwaka huu ikilinganishwa na miaka iliyopita. Nyuzijoto katika baadhi ya maeneo ya Uhispania ni zaidi ya 45 na joto hilo limepelekea misitu kuteketea moto.

Nchini Uingereza  joto pia limeongezka mwaka huu na kuvunja rekodi  ambapo mashariki mwa Uingereza kumeripotiwa nyuzi joto  40.3C na hivyo kupita kiwango cha juu cha hapo awali mnamo 2019.

Joto kali Ulaya limepelekea misitu iteketee moto

Kaskazini mwa Ureno, rubani alifariki wakati ndege yake ya kusaidia shughuli za zima moto ilipoanguka katika eneo la Foz Coa, karibu na mpaka wa Uhispania. Mamlaka ya Ureno inasema takriban watu 238 wamekufa kutokana na joto hilo kali katika wiki iliyopita.

Kwa sasa joto duniani limeongezeka kwa takriban nyuzi joto 1.1C tangu enzi ya viwanda ianze na halijoto itaendelea kuongezeka kama serikali kote ulimwenguni hazitafanya juhudi za kupunguza kiwango cha uzalishaji wa kaboni.