Jul 23, 2022 11:12 UTC
  • Kusainiwa mkataba wa mauzo ya nafaka kutoka Ukraine, mwanzo wa kutatua mgogoro wa chakula duniani

Jana Ijumaa, Ukraine, Uturuki na Umoja wa Mataifa zilitia saini makubaliano ya kutatua mgogoro wa nafaka duniani. Mkataba huo ulitiwa saini kati ya Oleksandr Kubrakov, Waziri wa Miundombinu wa Ukraine, Kholusi Akar Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu.

Kulingana na makubaliano hayo, udhibiti wa bandari za "Odessa", "Chornomorsk" na "Yuzhne" ambazo zitakuwa njia za kusafirishia nje nafaka, utakuwa chini ya mamlaka ya Ukraine. Muda wa makubaliano haya ni siku 120 na yanaweza kurefushwa. Iwapo makubaliano hayo yatatekelezwa, zaidi ya tani milioni 20 za nafaka zitasafirishwa kutoka kusini mwa Ukraine, jambo ambalo linaweza kusaidia juhudi za kupunguza mgogoro wa chakula na bei ya vyakula duniani. Inaonekana kuwa makubaliano haya yatakuwa hatua ya kwanza ya kutatua mgogoro wa chakula unaoisumbua dunia kwa sasa.

Kwa kuzingatia kwamba Russia na Ukraine zina jukumu muhimu katika kusambaza bidhaa za kimkakati za chakula kama vile ngano, mahindi na mafuta ya kula, makubaliano haya yanaweza kufungua njia ya kuanza tena mauzo ya bidhaa hizo kupitia bandari za Ukraine katika Bahari Nyeusi na kutoka huko hadi Bahari ya Mediterania na maeneo mengine ya dunia. 

Baada ya kuanza vita kati ya Russia na Ukraine mwishoni mwa Februari 2021, uwezekano wa kusafirisha bidhaa za chakula kutoka au kupitia Ukraine ulikuwa umefikia sifuri kutokana na mapigano yaliyokuwa yakiendelea katika maeneo ya pwani ya Ukraine, kama vile bandari ya Mariupol, na mvutano wa kijeshi kati ya pande hizo mbili kwenye mwambao wa kaskazini mwa Bahari Nyeusi. Wakati huo huo, vikwazo vya pande zote vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia vimesababisha kupungua kwa mauzo ya bidhaa hizo cha chakula, mbolea na nishati, suala ambalo limepelekea kujitokeza mgogoro wa chakula duniani. Itakumbukwa kuwa, zaidi ya nchi 50 zinategemea Russia na Ukraine kwa ajili ya kujidhaminia mahitajio yao ya ngano. Uhaba  au ongezeko la gharama ya ngano lina taathira mbaya kwa bei ya vyakula muhimu kama mkate na tambi. Bei ya aina nyingine za chakula imeongezeka kote duniani sambamba na kushadidi mgogoro wa Ukraine licha ya jitihada za nchi mbalimbali za kupata wauzaji mbadala wa bidha hizo muhimu. 

Katika suala hili, Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara juu ya shida ya chakula kutokana na ukosefu wa nafaka, na nchi za Magharibi pia zinaituhumu Russia kuwa inazuia usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine kuelekea kwenye masoko ya dunia, bila kutaja athari mbaya za hatua zao katika jambo hili. Moscow imekanusha vikali madai hayo.

Wakati huo huo, mafisa wa serikali ya Kiev wanaweka vizingiti na vikwazo vingi katika suala la mauzo ya nafaka kwa nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto nafaka katika bandari ya Mariupol na hatua ya jeshi la Ukraine ya kupandikiza mabomu ya kutega majini katika Bahari Nyeusi.

Russia imekanusha mara kwa mara tuhuma za Magharibi kwamba Moscow inatumia chakula kama silaha ya uharibifu dhidi ya nchi zingine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov ameyataja makubaliano ya Istanbul ya kusafirisha nafaka kutoka Bahari Nyeusi kuwa yanakadhibisha tuhuma zinazotolewa dhidi ya nchi yake na kuongeza kuwa, tabia na sera ya Marekani ya kutumia vibaya chakula kwa malengo ya kijiopolitiki ni jambo lisilokubalika na lisilo la kibinadamu. Sergei Lavrov amesema: "Nataka kusisitiza kwamba uvumi wa propaganda za Magharibi na Ukraine kwamba Russia "inasafirisha njaa" hauna msingi kabisa. Lavrov amesema, baada ya dunia kukumbwa na janga la corona, nchi za Magharibi zilitumia mfumo wa uchapishaji sarafu kubadili mtiririko wa uuzaji chakula na bidhaa nyingine kwa manufaa yao na hivyo kusababisha hali mbaya kwa nchi nyingine duniani ambazo zinategemea kununua bidhaa muhimu kutoka nje.  Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa vikwazo vya Magharibi dhidi ya nchi yake katika miezi ya hivi karibuni vimezidisha hali mbaya ya sasa.

Sergei Lavrov

Lavrov alikuwa akiashiria mchango haribifu wa nchi za Magharibi katika kuibuka mgogoro wa chakula duniani. Ukweli ni kwamba, kwa kuweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Russia, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya meli na bandari za nchi hiyo, Wamagharibi wamesababisha usumbufu mkubwa katika usafirishaji wa chakula, mbolea na bidhaa nyingine ambazo zinazotayarishwa na Russia kuelekea kwenye nchi nyingine duniani, hasa za Magharibi mwa Asia na Kaskazini mwa Afrika.

Tags