Watoto wahajiri nchini Marekani wapewa kazi za sulubu viwandani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86196-watoto_wahajiri_nchini_marekani_wapewa_kazi_za_sulubu_viwandani
Makumi ya watoto wahajiri wanatumikishwa na kupewa kazi za sulubu kwenye kiwanda kimoja cha kufua vyuma nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 23, 2022 06:53 UTC
  • Watoto wahajiri nchini Marekani wapewa kazi za sulubu viwandani

Makumi ya watoto wahajiri wanatumikishwa na kupewa kazi za sulubu kwenye kiwanda kimoja cha kufua vyuma nchini Marekani.

Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Reuters umefichua kuwa, kiwanda hicho kilichoko mjini Montgomery, jimboni Alabama, kusini mashariki mwa Marekani, kinatumikisha watoto wadogo raia wa kigeni, wakiwemo wa umri wa miaka 12.

Vyanzo vya habari vimeiambia Reuters kuwa, kiwanda hicho kina watoto zaidi ya 50 wanaofanya kazi kwa zamu tofauti, akthari yao wakiwa ni raia wa Amerika ya Latini.

Sakata hili la kutumikishwa watoto kiwandani nchini Marekani lilifichuka baada ya msichana wa miaka 13 aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni hiyo kutoweka tangu mwezi Februari mwaka huu. Baada ya polisi kuanzisha uchunguzi, walibaini kuwa binti huyo pamoja na ndugu zake wawili wa kiume wa miaka 12 na 15 walikuwa wakifanya kazi kwenye kiwanda hicho.

Kiwanda hicho cha SMART Alabama LLC kimepewa tenda ya kulipelekea vyuma na vipuri shirika la kuzalisha magari la Hyundai la Korea Kusini, tawi la jimbo la Alabama nchini Marekani.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, hivi sasa wasichana na wavulana milioni 160 wanatumikishwa katika maeneo mbalimbali duniani, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka mitano.

Umoja wa Mataifa umezitaka serikali za dunia kuimarisha mifumo ya ulinzi wa kijamii ili kufanikisha jitihada za kupambana na umaskini kwa ajili ya kutokomeza na kuzuia utumikishwaji wa watoto.