Kwa mara nyingine China yataka Syria iondolewe vikwazo
Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba kuna wajibu wa kuondolewa haraka vikwazo ilivyowekewa Syria kwani vikwazo hivyo vinakwamisha juhudi za kupeleka misaada ya kibinadamu nchini humo.
DAI Bing amesema hayo mbele ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulioitishwa kwa ajili ya kujadili suala la misaada ya kibinadamu nchini Syria na kuongeza kuwa, hatua ya baadhi ya nchi ya kuiwekea vikwazo kiholela Syria inakwamisha juhudi za kimataifa za kuwafikishia misaada ya kibinadamu watu wenye mahitaji ya dharura katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Amesema, vikwazo hivyo vinazorotesha juhudi za kujenga upya uchumi wa Syria na baya zaidi ni kwamba vinakwamisha jitihada za kimataifa za kufikisha misaada kwa wahitaji huko Syria.
Mwanadiplomasia huyo mkubwa wa China aidha ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka za kuondoa vikwazo dhidi ya Syria na pia amelitaka baraza la usalama la umoja huo kutangaza msimamo wake wa wazi kuhusu mateso wanayoendelea kupata wananchi wa Syria kutokana na vikwazo vya kidhulma walivyowekwa na nchi kama Marekani.
Mwaka 2011 Syria ilivamiwa na magenge ya kigaidi kutoka kila upande kwa uungaji mkono wa Saudia, Marekani na waitifaki wao na lengo lilikuwa ni kubadilisha milingano ya nguvu ya eneo hili kwa manufaa ya Israel. Zaidi ya wananchi milioni 12 wa Syria wamekuwa wakimbizi kutokana na uvamizi huo. Si hayo tu lakini pia wavamizi hao hao wa Syria wamewekwa vikwazo vingi vizito ambavyo vinakwamisha mno juhudi za kimataifa za kuwasaidia wahanga wa uhalifu huo wa nchi za Magharibi na vibaraka wao.