Aug 02, 2022 07:28 UTC
  • Biden athibitisha kuuawa kiongozi wa Al Qaeda Ayman al Zawahiri Afghanistan

Rais Joe Biden wa Marekani amethibitisha kuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda Ayman al Zawahiri ameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lililofanywa na jeshi la Marekani katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Biden, ambaye alikuwa kwenye karantini baada ya kukumbwa tena na ugonjwa wa Covid-19, ametangaza usiku wa kuamkia leo: "Tumemuua Ayman al Zawahiri Afghanistan, kiongozi wa kundi la Al Qaeda, ambaye amesababisha kuuawa Wamarekani wengi katika mashambulio tofauti."

Rais wa Marekani amesema, Al Zawahiri alichangia katika upangaji wa mashambulio ya Septemba 11, 2001 na akaongezea kwa kusema: Kwa miongo kadhaa, alikuwa mpangaji mkuu wa mashambulio dhidi ya Wamarekani.

Biden amesema, aliruhusu kufanyika shambulio makini la kumuua Ayman al Zawahiri na akadai kwamba, shambulio hilo halikusababisha madhara kwa yeyote katika watu wa familia yake wala raia yeyote wa kawaida. 

Biden

Rais huyo wa Marekani, ambaye nchi yake iliikalia kwa mabavu Afghanistan kwa muda wa miongo miwili na kusababisha umwagaji mkubwa wa damu katika nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi na hatimaye ikayaondoa ghafla na kwa aibu majeshi yake huku ikiiacha Afghanistan katika hali ya mchafukoge, amedai pia kuwa: Hatutaruhusu tena Afghanistan igeuzwe kuwa maficho ya magaidi."

Ayman al Zawahiri, kiongozi wa pili na wa mwisho wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ambaye Biden amethibitisha kuuawa kwake katika shambulio la droni, alishika uongozi wa kundi hilo mwaka 2011 baada ya kuuawa kiongozi wake wa kwanza Osama bin Laden.../

Tags