Ikulu ya Marekani yapigwa na radi, watu wanne wajeruhiwa vibaya
Watu wanne wamejeruhiwa vibaya baada ya radi kupiga eneo la nje la Ikulu ya Marekani, White House. Hayo ni kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo televisheni ya CNN ya Marekani.
Kwa upande wake shirika la habari la FARS limesema kuwa, maafisa wa zimamoto huko Washington, mji mkuu wa Marekani wamesema kuwa, watu hao waliopigwa na radi ni katika wale waliokimbilia eneo hilo kujikinga na mvua kali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanawake wawili na wanaume wawili wamejeruhiwa vibaya baada ya radi kupiga kwenye sehemu hiyo ya nje ya Ikulu ya Marekani.
Kwa upande wake, televisheni ya CNN imemnukuu msemaji wa kikosi cha zimamoto cha Washington DC, Vito Maggiolo, akithibitisha habari hiyo na kusema kuwa radi hiyo imepiga kwenye bustani ya Lafayette ya White House na kwamba watu hao wanne wamejeruhiwa vibaya na radi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa la Marekani watu takriban 20 huuliwa na radi nchini humo kila mwaka na mamia ya wengine hujeruhiwa.
Baadhi ya watu wanaopigwa na radi hubakia na kilema hadi mwisho wa umri wao hususan katika mifumo ya hisia ya miili yao.
Kwa upande wake mtandao wa habari wa Politico nao umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, bustani hiyo ya Lafayette ilifungwa kwa muda ili kushughulikia majeruhi na kuchukua tahadhari inayotakiwa.