Uhamishaji na usafirishaji nafaka kutoka Ukraine unaendelea vizuri
Kituo cha uratibu wa pamoja wa shughuli ya uhamishaji na usafirishaji wa shehena za nafaka kutoka Ukraine kimetangaza kuwa usafirishaji wa nafaka hizo unaendelea kwa kutumia meli nyingine tano za mizigo.
Kituo cha uratibu wa pamoja kinachosimamia operesheni ya usafirishaji nafaka kutoka Ukraine kilianzishwa kwa mujibu wa vifungu vya makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa Julai 22 mjini Istanbul, Uturuki kati ya Russia, Ukraine, Uturuki na Umoja wa Mataifa.
Uturuki, UN, Russia na Ukraine zilisaini makubaliano hayo kwa ajili ya kufunguliwa tena bandari za Odessa, Chernomorsk na Yuzhny nchini Ukraine ili kuweza kusafirisha shehena za nafaka zilizokuwa zimekwama katika bandari hizo kwa miezi kadhaa kutokana na vita vya Russia na Ukraine, vita ambavyo vingali vinaendelea kwa mwezi wa sita sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kituo cha uratibu wa pamoja, meli hizo tano zitaondoka leo katika bandari hizo tatu za Ukraine zikiwa zimebeba tani zaidi ya 161,000 za mahindi na bidhaa za chakula kuelekea Uturuki, China na Italia.
Hadi sasa meli nne zilizobeba tani zaidi ya 84,500 za nafaka zimeng’oa nanga katika bandari za Ukraine ikiwa ni katika utekelezaji wa makubliano ya kihistoria ya kuondoa kizuizi cha usafirishaji nafaka za Ukraine, hatua ambayo wengi wanaamini itasaidia kupunguza hatari ya baa la njaa duniani…/