Russia: Hatutasitisha operesheni ya kijeshi Ukraine mpaka tuyafikie malengo yetu yote
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87460-russia_hatutasitisha_operesheni_ya_kijeshi_ukraine_mpaka_tuyafikie_malengo_yetu_yote
Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema nchi hiyo haitasitisha operesheni yake maalumu ya kijeshi ndani ya ardhi ya Ukraine mpaka iyafikie malengo yake yote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 26, 2022 22:52 UTC
  • Russia: Hatutasitisha operesheni ya kijeshi Ukraine mpaka tuyafikie malengo yetu yote

Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema nchi hiyo haitasitisha operesheni yake maalumu ya kijeshi ndani ya ardhi ya Ukraine mpaka iyafikie malengo yake yote.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Dmitry Medvedev, ambaye pia ni rais wa zamani wa Russia ametangaza kuwa, lazima malengo yote ya operesheni maalumu ya kijeshi ya nchi hiyo ndani ya Ukraine yafikiwe. 

Medvedev amesisitiza kuwa, itapasa viongozi wa Ukraine waje wakiri kuhusu matokeo ya operesheni hiyo au yatokee mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo na baada ya hapo viongozi hao waje wakiri kuhusu matokeo ya operesheni hiyo ya kijeshi.

Vilevile Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema, utabiri wanaofanya Wamagharibi kuhusu vita vya Ukraine ni uongo.

Medani ya vita Ukraine

 

Medvedev amebainisha pia kuwa, Russia haiwezi kukubaliana na mtazamo kwamba shirika la kijeshi la Magharibi NATO linaweza kupiga kambi ndani ya ardhi ya Ukraine na akaongezea kwa kusema, uamuzi wa kufanya operesheni maalumu ya kijeshi ndani ya Ukraine ulipitishwa kwa sura ya kuchukua hatua ya kujihami kabla ya kushambuliwa ili Magharibi isije ikatangulia kuanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya Shirikisho la Russia.

Tangu vilipoanza vita na mapigano nchini Ukraine, hatua ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ya kushadidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Russia na kupeleka shehena za silaha nyepesi na nzito nchini Ukraine, si tu haijasaidia kutuliza hali ya mambo, bali imekoleza zaidi moto wa vita ndani ya nchi hiyo ya Ulaya.../