Russia: Hatutasimamisha vita hata Ukraine ikiacha azma ya kujiunga na NATO
Rais wa zamani wa Russia amesema iwapo Ukraine ingeliruhusiwa kujiunga na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO, Vita vya Tatu vya Dunia vingelikuwa vimeshaanza.
Dmitry Medvedev ambaye pia ni Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya LCI ya Ufaransa na kusisitiza kuwa, Russia haitasimamisha vita dhidi ya Ukraine hata kama Kiev itaachana na azma yake ya kujiunga na NATO.
Amesema operesheni za kijeshi za Russia dhidi ya Ukraine ndilo lilikuwa chaguo sahihi na laini zaidi kwa Moscow, na kwamba wanajeshi wa Russia wanalilenga tu jeshi la Ukraine.
Rais huyo wa zamani wa Russia amebainisha kuwa, "Miundombinu ya Ukraine ingelikuwa imeharibiwa kikamilifu, sawa na vituo vyake vya kufanya maamuzi na mamlaka za taifa hilo, lakini hatukufuata njia hiyo."
Kadhalika Medvedev ambaye ni mpambe wa karibu wa Rais Vladimir Putin wa Russia amekariri kuwa, Moscow haitasitisha operesheni yake maalumu ya kijeshi ndani ya ardhi ya Ukraine mpaka iyafikie malengo yake yote.
Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ameongeza kuwa, Moscow ipo tayari kufanya mazungumzo na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa masharti kadhaa, lakini hilo litategemea na namna mambo yatakavyoendelea kukunjuka katika operesheni zao kijeshi nchini Ukraine.