Mauzo ya silaha za Marekani yaongezeka katika utawala wa Biden
(last modified Sat, 10 Sep 2022 02:23:35 GMT )
Sep 10, 2022 02:23 UTC
  • Mauzo ya silaha za Marekani yaongezeka katika utawala wa Biden

Marekani imeendelea kushika nafasi ya kwanza duniani kwa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya bajeti ya masuala ya kijeshi, huku mauzo ya silaha za nchi hiyo yakiongezeka mno katika utawala wa Rais Joe Biden.

Shirika la Press TV limeripoti kuwa, Marekani mwaka jana ilitumia dola bilioni 801 kwa ajili ya bajeti ya jeshi lake, hiyo ikiwa ni asilimia 30 ya fedha zote zilizotengwa katika masuala yake ya kijeshi kote duniani 2021 (dola trilioni 2.1).

Kwa mujibu wa Taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI), Marekani imeongeza biashara yake ya silaha kwa nchi za Afrika, Ulaya na Asia Magharibi, na kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani.

Aidha kwa mujibu wa ripoti ya SIPRI, uvamizi wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh nchini Yemen, umeifanya Saudia kuwa mnunuzi mkubwa wa silaha katika eneo.

Mauzo ya silaha za Marekani kwa Saudia ni kinyume na ahadi ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo ya kukomesha vita vya Yemen na kuzuia uuzaji wa silaha nzito kwa utawala wa Riyadh. 

Maandamano ya kupinga kuuziwa silaha Saudia

Hii ni katika hali ambayo, utumiaji wa silaha za Marekani dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen unaendelea kukosolewa vikali na watetezi wa haki za binadamu katika kona mbalimbali za dunia.

Hivi karibuni pia, utawala wa Rais Joe Biden ulipasisha pendekezo la kuiuzia Taiwan silaha za dola bilioni 1.1, yakiwemo makombora 60 ya kulenga manowari na 100 ya anga kwa anga. Mpango huo umekosolewa vikali na Beijing inayosisitiza kuwa, mawasiliano yoyote ya kijeshi na Taipei ni ukiukaji wa kanuni ya "China Moja".