Katibu Mkuu wa NATO: Mzozo wa Ukraine hautamalizika karibuni
Sep 17, 2022 02:51 UTC
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema mzozo kati ya Russia na Ukraine hautaisha hivi karibuni, licha ya kile alichokiita shambulio "athirifu" la kujibu mapigo lililofanywa na vikosi vya Kiev dhidi ya wanajeshi wa Moscow.
Akizungumza katika mahojiano na Redio ya BBC Stoltenberg amebainisha kwa kusema: "inatia moyo sana kuona kwamba vikosi vya jeshi la Ukraine vimeweza kutwaa tena maeneo na kushambulia safu za vikosi vya jeshi la Russia."
Hata hivyo, amesisitiza kwa kusema, ni muhimu kuelewa kwamba "huu sio mwanzo wa mwisho wa vita, inatupasa tujiandae kwa safari ndefu."
Matamshi ya Stoltenberg yanakuja baada ya Russia kutangaza kuwaondoa wanajeshi wake katika maeneo kadhaa kaskazini mashariki mwa Ukraine, ukiwemo mji wa Izium. Moscow inasisitiza kwamba, hatua hiyo imechukuliwa ili kuimarisha vikosi vyake huko Donetsk, wakati Kiev inasherehekea kujiondoa kwa vikosi vya Russia kama ushindi.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa NATO alitahadharisha kwamba Ukraine inaweza "kukoma kuwepo" kama taifa huru isipokuwa kama itaendeleza mapambano yake dhidi ya Russia, ambayo anadai, inataka "kuidhibiti Ukraine."
Stoltenberg amerudia tena wito wake kwa mataifa ya Magharibi kuendelea kuiunga mkono Ukraine kwa kuipelekea nchi hiyo misaada zaidi ya kijeshi, na pia kuwapa wanajeshi wa Kiev pamoja na mambo mengine sare za kutosha kwa ajili ya msimu ujao wa baridi, majenereta na mahema.
Moscow imezitaka mara kwa mara nchi za Magharibi ziache "kuishindilia" Ukraine silaha na vifaa vingine vya kijeshi, ikisisitiza kwamba kufanya hivyo kunarefusha muda wa umwagaji damu tu bila kubadilisha matokeo na hatima ya mzozo huo.../
Tags