174 waaga dunia katika mkanyangano kwenye uwanja wa soka Indonesia
(last modified Sun, 02 Oct 2022 07:34:07 GMT )
Oct 02, 2022 07:34 UTC
  • 174 waaga dunia katika mkanyangano kwenye uwanja wa soka Indonesia

Kwa akali watu 174 wamepoteza maisha baada ya mashabiki wa timu hasimu za mpira wa miguu kushambuliana katika uwanja wa soka nchini Indonesia.

Inaarifiwa kuwa, mashabiki wa klabu ya soka ya Arema jana Jumamosi waliingia kwa hasira katika uwanja wa soka wa Kanjuruhan jijini Malang, baada ya timu yao kuchabangwa mabao 3-2 na Persebaya Surabaya, hicho kikiwa kichapo cha kwanza baada ya kupita karibu miongo miwili.

Askari polisi walilazimika kuingilia kati kuzima fujo hizo kwa kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi, baada ya maafisa wenzao wawili kuuawa kwenye ghasia hizo.

Hata hivyo machafuko yalishtadi na ikawa hali ya mshike mshike uwanjani hapo. Polisi ya Indonesia inasisitiza kuwa, akthari ya waliopoteza maisha walikufa kutokana na mkanyagano.

Awali Kamanda Mkuu wa Polisi eneo la Java Mashariki, Nico Afinta alisema watu 127 wameaga dunia kwenye mkasa huo, wakiwemo maafisa wawili wa polisi.

Mshike mshikeke uwanjani Indonesia

Waziri wa Michezo na Vijana wa Indonesia, Zainudin Amali ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo lililopelekea makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Shirikisho la Soka Indonesia  (PSSI) limesimamisha mechi zote za kandanda kwa muda wa wiki moja, sambamba na kuipiga marufuku timu ya Arema FC kuwa mwenyeji wa mechi za soka kwa muda wote uliobaki msimu huu.

 Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Mochamad Iriawan ameomba radhi kwa familia za wahanga wa tukio hilo, na kuongeza kuwa watatuma maafisa wao kwenda mjini Malanga kuchunguza kiini cha mkasa huo.