Wataliano waandamana dhidi ya serikali; wataka kutatuliwa mgogoro wa nishati
Wananchi wa Italia wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, kulalamikia hatua ya serikali ya nchi hiyo kushindwa kutafutia ufumbuzi mgogoro wa nishati unaowakabili.
Katika mji mkuu wa Rome, maandamano hayo yameongozwa na wanafunzi wa sekondari, ambao mbali na kulalamikia hali ngumu ya maisha na mgogoro wa nishari, wameitaka serikali iwekeze ipasavyo katika sekta ya elimu.
Jana Jumamosi, mamia ya wananchi wa Italia wakingozwa na wanafunzi wa shule za upili walikusanyika nje ya Wizara ya Elimu mjini Rome, kulaani hatua ya serikali ya kupunguza bajeti ya sekta ya elimu ndani ya miongo miwili iliyopita, na kufanya Italia kushuhudia ongezeko kubwa zaidi barani Ulaya la wanafunzi kutomaliza shule ya upili.
Wananchi wa Italia kama nchi nyingi za Ulaya, wamekuwa wakifanya maandamano katika siku za hivi karibuni kulalamikia gharama ya juu ya maisha, huku wakishinikiza kutafutia ufumbuzi mgogoro wa nishati.
Usambazaji wa gesi ya Russia kuelekea barani Ulaya umepungua kwa kiasi kubwa sana kutokana na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow, baada ya Russia kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine.
Kupungua kwa mauzo ya gesi ya Russia kwa Italia kumesababisha watu laki tano kukosa ajira nchini Italia. Iwapo Russia itasitisha kikamilifu kusafirisha gesi barani Ulaya kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, basi Italia itakabiliwa na uhaba wa gesi kwa mita za ujazo zipatazo bilioni 6.4.