Russia yaionya vikali Israel dhidi ya kuipa silaha Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i89408-russia_yaionya_vikali_israel_dhidi_ya_kuipa_silaha_ukraine
Rais wa zamani wa Russia ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na kuutaka usithubutu kuipa silaha Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2022 04:10 UTC
  • Russia yaionya vikali Israel dhidi ya kuipa silaha Ukraine

Rais wa zamani wa Russia ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na kuutaka usithubutu kuipa silaha Ukraine.

Dmitry Medvedev ambaye ni Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ametoa indhari hiyo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram na kusisitiza kuwa, kuipa silaha Ukraine ni hatua hatari ambayo imeharakishwa na ambayo haijazingatia matokeo yake mabaya.

Amebainisha kuwa, utawala haramu wa Israel unajiandaa kuipa Ukraine silaha, na iwapo hilo litatokea, uhusiano baina ya Moscow na Tel Aviv utasambaratika.

Mwanasiasa huyo wa Russia ameeleza bayana kuwa, inashangaza Israel inataka kuwapa silaha watu wanaotumia nembo za Kinazi, na wanaopigania fikra na itikadi za Ujerumani ya Kinazi, licha ya kuwa fikra hizo zimewahi kutumia huko nyuma dhidi ya jamii mbalimbali ikiwemo ya Wayahudi.

Wamagharibi wanavyorundika silaha nchini Ukraine ili kushadidisha vita

Kabla ya hapo, Medvedev alisema fikra, mienendo na misimamo ya Rais wa Ukraine inafanana na ya mtawala wa zamani wa Ujerumani ya Manazi, Adolf Hitler.

Alisema hayo wakati akijibu bwabwaja za Volodymir Zelensky, Rais wa Ukraine ambaye alikuwa ametoa mwito kwa nchi zote za Magharibi kuwapiga marufuku raia wote wa Russia.

Rais wa zamani wa Russia alisisitiza kuwa, misimamo hiyo ya Zelensky inashabihiana na ile iliyochukuliwa na Adolf Hitler katika Vita vya Pili vya Dunia ambavyo vilisababisha zaidi ya watu milioni mbili kuuawa.