Lavrov asisitiza kushirikiana na Iran, China, Uturuki na India
Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia jana Ijumaa alisisitiza kuwa kuna umuhimu Moscow kushirikiana na Tehran, Beijing, Ankara, New Delhi na nchi nyingine za pambizoni mwa bahari ya Kaspi.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa maeneo ya Russia, Sergei Lavrov amesema: kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Russia na Iran, China, Uturuki, India na nchi nyingine za kandokando ya bahari ya Kaspi, na kwamba Moscow inataka kuanzisha mfumo wa dunia wa kambi kadhaa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza kuwa, Moscow inategemea kupanua uhusiano na nchi za kundi la BRICS na kwamba, ni muhimu kushirikiana na Iran, Uturuki na nchi nyingine za kandokando ya bahari ya Kaspi.
Lavrov aidha amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Russia, Iran na Uturuki na akaongeza kwamba Moscow ina hamu ya kusaini mikataba zaidi kati yake na India na China.
Hii ni katika hali ambayo muungano kati ya Moscow, Tehran, Beijing, Ankara na New Delhi umeimarika sana hivi sasa kuliko huko nyuma baada ya Russia kuanzisha oparesheni za kijeshi huko Ukraine Februari 24 mwaka huu; ambapo nchi za Magharibi khususan Marekani na Uingereza zilifanya jitihada kuu za kuitenga Russia kimataifa kupitia kushadidisha vikwazo dhidi ya nchi hiyo na kuipatia Kiev silaha nyepesi na nzito.
