Duru ya pili ya ziara ya Zarif barani Ulaya
Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameanza duru yake ya pili ya safari yake barani Ulaya kwa kuitembelea Norway ambapo anatazamiwa kushiriki kikao cha "Oslo Forum".
Zarif leo Jumatatu amewasili mjini Oslo akiwa pamoja na Sayyid Abbas Araqchi, Majid Takhe-Ravanchi na Hussein Jaberi Ansari maafisa wa ngazi za juu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran. Viongozi wa nchi mbalimbali akiwemo John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na Bi Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya pia wanashiriki kwenye kikao hicho.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepangiwa kuhutubia kikao hicho ambacho kinafuatilia masuala ya kibinadamu katika ngazi za kimataifa. Kikao cha Oslo kinatambulika kama kongamano kuu linalowakutanisha wasuluhishi wa mizozo ya kivita, wachukuaji maamuzi wa za juu na weledi wa mambo.
Baada ya kuhudhuria kikao hicho cha Norway, Muhammad Javad Zarif ataelekea Ujerumai ambapo atakuwa na mazungumzo huko Berlin na Frank Walter Stainmeier Waziri mwenzake wa Ujerumani katika safari yake hiyo ya masaa kadhaa nchini humo. Mazungumzo ya Zarif na Stainmeier yatahusu uhusiano wa pande mbili na masuala mengine ya kieneo pia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifanya ziara katika nchi nne za Sweden, Finland, Lithuania na Poland katika duru ya kwanza ya safari yake barani Ulaya yapata karibu mwezi mmoja uliopita. Akiwa katika duru ya pili ya safari yake barani Ulaya, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atakuwa na mazungumzo yatakayojadili ushirikiano wa pande mbili na wa pande kadhaa pia. Mazungumzo hayo yametajwa kuwa na umuhimu kwa ajili ya kuandaa ramani ya njia ya kuimarisha uhusiano wa kisaisa na kiuchumi kati ya Iran na nchi za Ulaya baada ya kufikiwa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Hii ni kwa sababu hali ya sasa ya kiuchumi ya Iran imebadilika baada ya kufikiwa mpango wa JCPOA na kuondolewa maazimio ya Baraza la Usalama na ya Bodi ya Magavana ya Wakala wa IAEA , ambapo Iran hivi sasa imekuwa na ongezeko la uzalishaji bidhaa na imeweza kurudi kwa mafanikio katika masoko ya mafuta ya kimataifa. Kuzingatiwa malengo ya uchumi wa kimuqawama katika mikataba na maamuzi ya kiuchumi yanayochukuliwa katika uwanja huo pia, kuna nafasi kuu katika kuainisha kiwango na aina ya mahusiano ya kiuchumi inayotaka kuwa nayo Iran na nchi nyingine.
Sekta ya mafuta na gesi, uwekezaji vitega uchumi wa pamoja katika nyanja za viwanda, kuimarisha shughuli za sekta binafsi, ushiriki wa kisiasa na kieneo, ni miongoni mwa masuala ambayo yatachunguzwa na kujadiliwa katika safari ya Zarif huko Norway na Ujerumani.
Kwa msingi huo, udiplomasia wa kieneo wa Iran kuhusu kupatiwa ufumbuzi matatizo ya kieneo, ni moja ya kadhia zenye umuhimu katika mazungumzo ya kisiasa kati ya Iran na nchi za Ulaya. Kuhusiana na suala hilo, mapendekezo na mitazamo itakayowasilishwa na Muhammad Javad Zarif kupitia hotuba atakazotoa kwenye kikao cha Oslo, yatakuwa na umuhimu mkubwa.
Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi nyingine wanachama wa kundi la 5+1 wameahidi kufuatilia utekelezaji kamili wa makubaliano ya JCPOA katika mazungumzo yatakayofanywa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na Federica Mogherini. Hata hivyo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge na Baraza la Usalama wa Taifa la Iran tayari zimebuni hatua mbadala mkabala na hatua za upande wa pili ambazo huenda zikahesabiwa kuwa ni hatua za ukiukaji au zenye kukinzana na mapatano yaliyofikiwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekuwa ikifuatilia kwa makini utekelezaji wa mpango wa JCPOA na kulinda haki za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu kufikiwa mazungumzo ya nyuklia na mpango kamili wa pamoja wa utekelezaji. Katika uwanja huo, utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia na harakati nyingine za makundi yanayofahamika huko Marekani na Canada, zimekuwa zikifanya kila njama kukwamisha makubaliano hayo kwa kuionyesha Iran kuwa ni tishio na kwamba si mahala salama kwa wawekezaji wa nje. Pande hizo aidha zimeandaa mpango wa kuionyesha Iran kuwa ni tishio kwa kutoa madai yasiyo na msingi kwamba Iran inaunga mkono ugaidi na kukiuka haki za binadamu. Kwa msingi huo, ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran barani Ulaya inafanyika kwa lengo la kuzima njama na harakati hizo zenye malengo tofauti.