Dec 27, 2022 07:20 UTC
  • Moscow yatoa onyo baada ya Washington kutishia kumuua Rais wa Russia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametoa indhari baada ya maafisa 'wasiojulikana' wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kutoa vitisho vya kumuua Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo.

Katika mahojiano na shirika la habari la TASS, Sergei Lavrov amesema, "Washington imekubuhu, maafisa wasiojulikana wa Washington wamepaza sauti na kutishia kuishambulia vikali Kremlin (Ikulu ya Rais wa Russia)." 

Amesema vitisho hivyo ni sawa na kutishia kumuua kigaidi Rais wa Russia. Amebainisha kuwa, "Iwapo mawazo ya aina hii yatatiliwa maanani na mmoja, basi anapaswa kutafakari vyema juu ya matokeo mabaya ya mipango ya aina hiyo."

Lavorv ameashiria vitisho vinavyotolewa mara kwa mara na viongozi wa nchi za Magharibi dhidi ya Russia na kueleza bayana kuwa, Wamagharibi wamepoteza heshima machoni pa walimwengu kwa vitisho na bwabwaja zao.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amekumbusha kauli ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truss aliyesema kadamnasi kwamba serikali yake haitasita kutumia silaha za maangamizi za nyuklia, iwapo nchi hiyo italazimika kufanya hivyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov

Truss akijibu swali aliloulizwa wakati wa kampeni za kugombea uwaziri mkuu iwapo atakuwa tayari 'kobonyeza kitufe' na kuisawazisha dunia ikilazimu, alisema, "Nadhani ni jukumu muhimu la Waziri Mkuu, na nipo tayari kufanya hivyo."

Russia ilitangaza ilipoanzisha operesheni maalumu nchini Ukraine mapema mwaka huu kwamba, itasitisha operesheni hiyo ya kijeshi iwapo itapewa dhamana na kuhakikishwa kwamba Kiev si tishio la kijeshi, na vilevile kuondoka madarakani Wanazi Mamboleo katika nchi hiyo ya Ulaya Mashariki.  

 

Tags