Feb 02, 2023 12:11 UTC
  • Warepublican waanza mchakato wa kumuondoa Ilhan Omar katika Kamati ya Mambo ya Nje ya Congresi kwa kuikosoa Israel

Wanachama wa Republican katika Baraza la Wawakilishi la Marekani wanajiandaa kupigia kura muswada wa kumuondoa mwakilishi wa Kidemokrati, Ilhan Omar kwenye Kamati ya Masuala ya Kigeni, siku chache baada ya kuondolewa katika Kamati ya Masuala ya Afrika, kutokana na kukosoa ukatili na mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina.

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Kevin McCarthy alikuwa amethibitisha juzi Jumanne, katika mahojiano yake na televisheni ya CNN, kwamba wamepata asilimia ya kutosha ya kura kumuondoa mbunge huyo Mwislamu katika Kamati ya Masuala ya Nje kwa sababu ya ukosoaji wake wa hapo awali dhidi ya Israeli, jambo ambalo lilitambuliwa kuwa ni upinzani dhidi ya Mayahudi.

Ijumaa iliyopita, Warepublican walio wengi katika Baraza la Wawakilishi walimfukuza Ilhan Omar kwenye Kamati ya Masuala ya Afrika ya Kongresi.

Kuhusiana na juhudi za Kevin McCarthy Spika wa Bunge la Marekani za kutaka kumuondoa katika Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya bunge hilo, Bi Ilhan Omar mwenye asili ya Somalia amesema, baadhi ya wajumbe wa chama cha Republican wanaafikiana na kampeni chafu za chuki dhidi ya Uislamu.

Mbunge huyo wa Kiislamu katika Kongresi ya Marekani ameongeza kuwa, wanachama wa chama cha Republican kama Kevin McCarthy hawakubaliani kabisa na suala la kuweko mbunge Mwislamu katika Kongresi ya Marekani ambaye atakuwa sauti ya Waislamu wengine.

Ilhan Omar

Kadhalika amesema, akthari ya wajumbe wa chama chah Republican wanaamini kuwa, Mwislamu, mhajiri na Mwafrika hapaswi kabisa kuwa mwakilishi katika Bunge la Marekani seuze awepo katika Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya bunge la nchi hiyo.

Ilhan Omar, mwanasiasa wa Marekani mwenye asili ya Kisomali, ni mwanachama wa chama cha Democratic, na alishinda ubunge wa jimbo la Minnesota katika Baraza la Wawakilishi mnamo Novemba 2016, na kuwa mwanamke wa kwanza Mwislamu anayevaa hijabu katika Bunge la Marekani.

Tags