Meya wa Barcelona avunja uhusiano na Israel, aitetea Palestina
(last modified Fri, 10 Feb 2023 02:25:24 GMT )
Feb 10, 2023 02:25 UTC
  • Meya wa Barcelona avunja uhusiano na Israel, aitetea Palestina

Jiji la Barcelona la kaskazini mashariki mwa Uhispania limetangaza kusimamisha uhusiano wake na utawala haramu wa Israel.

Ada Colau, Meya wa Barcelona ametangaza habari ya kukata uhusiano na Tel Aviv kwa muda usiojulikana, kulalamikia sera kandamizi za Israel dhidi ya Palestina.

Katika barua yake kwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Meya wa Barcelona amesema amefikia uamuzi wa kusimamisha uhusiano na Tel Aviv, hadi pale Israel itakapokomesha ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina.

Sehemu moja ya barua ya Ada Colau kwa Netanyahu inasema: Nimeamua kusimamisha kwa muda uhusiano na Israel, mpaka pale mamlaka (za utawala huo) zitakapositisha ukanyagaji wa kimpangilio wa haki za Wapalestina, na zifungamane na sheria za kimataifa na maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa. 

Maandamano ya kuisusia Israel na kuitetea Palestina huko Israel

Meya huyo wa mji wa Barcelona, ambayo ni makao makuu ya eneo la Catalonia nchini Uhispania amesema hawezi kunyamaza kimya na kufumbia macho jinai wanazofanyiwa Wapalestina na utawala pandikizi wa Israel.

Kwa muda mrefu sasa, vyama kadhaa vya siasa nchini Uhispania vimekuwa vikiendeleza kampeni kubwa ya kuususia utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa lengo la kuwahami na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Vyama vya siasa vya Uhispania vilivyoanzisha kampeni hiyo miaka kadhaa iliyopita vinataka kupigwa marufuku kushirikiana na mashirika ya Israel au kununua bidhaa za mashirika hayo. Kampeni hiyo inasisitiza pia kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina.