Mar 25, 2023 02:18 UTC
  • Onyo la Russia kuhusu kuzuka vita vya nyuklia kufuatia ongezeko la kutumwa silaha za Magharibi nchini Ukraine

Dmitry Medvedev, Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Kitaifa la Russia, ameonya juu ya uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia, akisema kuendelea kutumwa silaha nchini Ukraine kunaongeza maradufu uwezekano wa kuibuka hivi karibuni vita vya nyuklia karibu katika eneo.

Akijibu swali kupitia mahojiano, iwapo hatari ya kutokea vita vya atomiki imepungua au la, Medvedev amesema uwezekano wa kutokea vita hivyo si tu haujapungua bali umeongezeka zaidi. Amesema kila mara silaha za nchi za Magharibi zinapoendelea kutumwa Ukraine uwezekano wa kutokea vita hivyo nao unaongeza.

Onyo la kiongozi huyo wa ngazi za juu wa usalama wa Russia limetolewa kufuatia kuongezeka mwenendo wa kutumwa silaha za nchi za Magharibi huko Ukraine kwa lengo la kuendeleza vita dhidi ya serikali ya Moscow. Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na harakati nyingi katika uwanja huo. Kati ya harakati hizo ni kwamba Marekani tayari imetangaza msaada wa silaha wa dola milioni 350 kwa Ukraine, na nchi mbili za Ulaya Mashariki, yaani Poland na Slovakia, zinapanga kulipa jeshi la anga la Ukraine ndege 14 za kivita aina ya MiG-29 katika awamu ya kwanza ya msaada wa kijeshi wa nchi mbili hizo kwa serikali ya Kyiv.

Challenger 2

Lakini silaha zenye utata zaidi ambazo nchi za Magharibi zinapanga kuzituma Ukraine ni makombora na risasi zilizotengenezwa kwa urani hafifu. Annabelle Goldie, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Uingereza ametangaza kuwa London hivi karibuni itatuma nchini Ukraine silaha zenye urani iliyohafifishwa. Kwa mujibu wa kauli yake, sehemu ya silaha zinazotumiwa na vifaru aina ya Challenger 2 ambazo Uingereza itazituma Ukraine zina madini ya urani iliyohafifishwa. Risasi zilizotengenezwa kwa urani iliyohafifishwa zinaweza kupenya na kuharibu kirahisi vifaru na magari ya kivita.

Mbali na hayo, vumbi linalotokana na kufyatuliwa risasi hizo na matokeo ya baada ya kulipuka kwake yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya mwanadamu, hasa kwenye mapafu na viungo vingine muhimu mwilini. Kabla ya hapo, jeshi la Marekani lilitumia mabomu na risasi za urani iliyohafifishwa wakati wa uvamizi na kukaliwa kwa mabavu Iraq, suala ambalo lilikuwa na madhara makubwa kwa wanajeshi wa Marekani na vile vile watu wa Iraq, na wakati huo huo kusababisha uchafuzi mkubwa wa mionzi katika maeneo ambayo silaha hizo zilitumika.

Suala la kutumwa silaha za aina hiyo huko Ukraine limeikasirisha sana Russia, kwa kadiri kwamba viongozi mbalimbali wa nchi hiyo wamelalamikia vikali hatua hiyo ya Uingereza na kuionya kuhusu hatari ya kutekelezwa kivitendo hatua hiyo. Rais Vladimir Putin wa Russia amelaani vikali mpango wa Uingereza wa kutuma Ukraine vifaru nyenye uwezo wa kutumia silaha zilizotengenezwa kwa urani iliyohafifishwa na kuonya kuwa bila shaka Moscow itatoa jibu linalonasibiana na hatari hiyo. Kuhusu suala hilo, Putin amesema: "Nchi za Magharibi ndizo zitakuwa za kwanza kutumia silaha zenye mada za nyuklia." Awali, Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, alionya kuhusu hatari ya kukaririwa "hali ya Yugoslavia" nchini Ukraine na kusema kutumika silaha zenye urani iliyohafifishwa kunaweza kusababisha saratani na uchafuzi wa mazingira.

Katika msimamo wake wa karibuni kuhusiana na suala hilo, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka mzozo wa Ukraine kutokana na uamuzi wa London wa kutuma nchini humo silaha zenye urani iliyohafifishwa. Amesema matumizi ya mabomu yenye urani iliyohafifishwa nchini Ukraine yatadhuru kilimo cha nchi hiyo.

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Kwa hakika, taratibu Wamagharibi wamepuuza sheria na viwango vyote walivyoweka kuhusu silaha zinazopaswa kutumwa Ukraine ikiwa ni katika kutekeleza nadharia yao inayosema 'lengo huhalalisha mbinu inayotumika kulifikia'. Hivyo uamuzi wao wa kutuma Ukraine vifaru vilivyo na uwezo wa kutumia silaha zilizotengenezwa kwa urani hafifu na vile vile  uzoefu mchungu wa kutumika silaha za aina hiyo katika vita vya Iraq, ambazo zimekuwa na madhara makubwa kwa afya ya mwanadamu na mazingira anamoishi, unatekelezwa katika muktadha huo huo. Kwa maneno mengine yaliyo wazi zaidi ni kuwa, nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani na Uingereza, zimeamua kutumia silaha na zana zozote zitakazosababisha uharibifu na maafa makubwa zaidi kwa vikosi vya Russia huko Ukraine, bila kujali iwapo silaha hizo ni halali kisheria au la. Katika muktadha huo, wanachama 4 wa chama cha Republican wa Congress ya Marekani wametuma barua kwa White House, wakitaka kutumwa mabomu ya vishada huko Ukraine, ambayo tayari matumizi yake yamepigwa marufuku kimataifa.

Tags