Apr 10, 2023 07:55 UTC
  • Polisi ya Canada yamfungulia mashtaka ya uhalifu wa chuki aliyeshambulia msikiti, kuchana Qur'ani

Polisi ya Canada imetangaza kuwa imemkamata na kumfungulia mashtaka mwanamume mmoja kwa kile kilichoelezwa kuwa ni "tukio la chuki" katika msikiti mmoja wa jimbo la Ontario Alhamisi iliyopita, baada ya kuhujumu Waislamu, kuwatishia na kuwatusi.

Taarifa iliyotolewa na polisi wa York imesema kwamba tukio hilo lilitokea katika mji wa Markham, huku mshukiwa, Sharan Karunakaran, 28, akikamatwa huko Toronto.

Waziri wa Biashara wa Canada, Mary Ng amelaani shambulio hilo la chuki dhidi ya Uislamu lililolenga msikiti mmoja eneo la Markham, Ontario, wakati mtuhumiwa huyo alipovunjia heshima nakala ya Qur'ani Tukufu na kujaribu kuwashambulia waumini kwa gari.

Waziri mary Ng alisema kwamba amefadhaishwa sana kusikia uhalifu wa chuki na tabia ya ubaguzi dhidi ya Jamii ya Kiislamu ya Markham na akatangaza mshikamano wake na Waislamu wa Markham na Canada kwa ujumla.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Kiislamu ya Markham (ISM), ambayo ni moja ya taasisi kongwe na kubwa zaidi za Kiislamu nchini Canada, ilisema kuwa Alhamisi iliyopita mtu mmoja alifika eneo hilo akiwa na gari ambapo aliingia msikitini na kurarua nakala ya Qur'ani Tukufu. Ilisema mbaguzi huyo aliyekuwa akitoa nara za ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu, alijaribu pia kuwagonga Waislamu waliokuwepo eneo hilo kwa gari lake.

Hata hivyo inasikitisha kuwa Polisi ya Canada imeficha au imejizuia kueleza tukio la kuchanwa na kuraruliwa kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika hujuma hiyo. 

Shambulio dhidi ya kituo na msikiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Markham (ISM), limefanyika katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, ambao unatambuliwa kuwa mwezi mtakatifu zaidi katika kalenda ya Kiislamu.

Canada ni mojawapo ya vituo vinavyoibuka kwa kasi vya chuki dhidi ya Uislamu (islamophobia) na uhalifu wa chuki kote ulimwenguni.

Utafiti mpya uliofanywa na Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada (NCCM) umeonyesha kuwa, hujuma za chuki dhidi ya Waislamu nchini humo ziliongezeka kwa asilimia 71 mwaka 2021.

Tags