Sisitizo la kuimarishwa BRICS kwa kupanuliwa muundo wa usalama
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amehutubia kikao cha mabalozi wa nchi za jumuiya ya BRICS zinazojumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini mjini Moscow, akisisitiza haja ya kuwepo juhudi za pamoja za kukabiliana na vitendo vya uharibifu vya nchi za Magharibi ambazo lengo lao ni kuharibu muundo wa usalama.
Katika kikao hicho, washiriki wamesisitiza mshikamano wao na mfumo wa ulimwengu wa kambi nyingi unaoheshimu sheria za kimataifa na uchaguzi huru wa njia ya maendeleo. Washiriki pia walijadili ustawi na njia za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati ndani ya kundi la BRICS, hasa vipaumbele vilivyowekwa na Afrika Kusini.
Sera ya ulimwengu wa kambi kadhaa (multilateralism) badala ya kambi moja (unilateralism) imekuwa ikipewa umuhimu na nchi nyingi duniani kwa miaka mingi. Nchi mbalimbali zimejaribu kuwa na mabaraza katika nyanja tofauti za kisiasa na kiuchumi kwa kuunda jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa. Katika suala hili, zaidi ya muongo mmoja umepita tangu kuanzishwa kwa kundi la BRICS, muungano unaoongozwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani.

Wanachama wa kundi hili lililoanzishwa kutokana na kuungana nchi za Russia, India, China, Brazil na Afrika Kusini, wameongeza ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa hususan katika miaka ya hivi karibuni. Nchi hizo zimekuwa na utendaji mzuri, na wachambuzi wengi sasa wanasema muungano huo unakabiliana na miungano ya Ulaya na Marekani. Takwimu zilizochapishwa zinaonyesha kuwa, nchi za BRICS ni wazalishaji muhimu zaidi wa bidhaa, huduma na malighafi duniani. Kwa sasa nchi za kundi la BRICS zina 42% ya watu, 30% ya ardhi, 26% ya Pato la Taifa na 20% ya biashara ya bidhaa ya dunia.
Muungano huo umekuwa muhimu sana hasa kutokana na kuzuka kwa vita vya Ukraine na kambi mpya za kisiasa. Sasa, nchi mbalimbali zinazotarajiwa kuwa nguvu kubwa za kiuchumi na kisiasa katika siku za usoni, chini ya jina la BRICS, zinataka kuunda utaratibu mpya unaozingatia muundo wa kambi nyingi ambao unatoa kipaumbele kwa suala la kuvuka kipindi cha ubepari wa mtindo wa Kimagharibi katika mfumo wa kimataifa. Nchi hizi zinataka kuimarisha ushirikiano sio tu katika masuala ya kiuchumi, bali pia katika masuala ya kisiasa na kiusalama.
Feng Xingke, Katibu Mkuu wa Jukwaa la Fedha Duniani na Mkurugenzi wa Kituo cha BRICS na Mfumo wa Kimataifa, amesema: Katika hali ya sasa, jukumu la BRICS katika usalama wa kimataifa limekuwa dhahiri na muhimu zaidi.
Hivi sasa wanachama wa BRICS wana uhusiano mkubwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kijeshi na kiusalama, silaha, nyanja za kisiasa na kidiplomasia, na wanasisitiza haja ya kuimarishwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kutatua matatizo mbalimbali na pia kukabiliana na ukiritimba wa nchi za Magharibi na sera za uchokozi za Marekani katika masuala tofauti.
Utendaji mzuri wa kundi hili umekuwa sababu ya nchi nyingine kuomba uanachama katika jumuiya ya BRICS. Kuhusiana na hili, Algeria, Argentina na Iran tayari zimetuma maombi ya kujiunga na BRICS, na Saudi Arabia, Uturuki na Misri pia zimetangaza nia yao ya kujiunga na kundi hili.
"Fawaz Kasab Al-Anzi", mchambuzi wa masuala ya uchumi anasema: BRICS ni muungano wa kimataifa wa kiuchumi na unajumuisha nchi zenye uchumi mkubwa na mapato ya juu ya kitaifa katika ngazi ya kimataifa. Kwa hakika, kundi la BRICS linalenga kuunda mfumo wa kambi nyingi duniani badala ya kambi moja, ambao unazipa nchi wanachama aina ya uwiano na ubadilishanaji wa haraka wa biashara ili kufufua uchumi wao.