FAO: Wanawake wanashikilia nafasi ya pambizoni katika uzalishaji wa chakula
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limesema katika ripoti yake nadra kuwahi kutolewa kuhusu kukosekana kwa usawa wazi katika sekta hiyo.
FAO imesema katika ripoti yake hiyo kuwa, wanawake wanamiliki ardhi ndogo, wanapata fedha kidogo na wakati huo huo wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na migogoro. Wakati huo huo wanawake wanashikilia nafasi ya pembezoni katika uzalishaji wa chakula licha ya kuwa ni watu muhimu katika kulisha walimwengu.
Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) imeendelea kubainisha kuwa: Kuanzia mashambani hadi uzalishaji wanawake ndio wanaopambana na mazingira mbalimbali ya kazi ambayo mara nyingi huwa magumu zaidi kulinganisha na yale wanayokabiliana nayo wanaume.
Qu Dongyu Mkurgenzi Mkuu wa FAO amesema ili kukabiliana na ukosefu huu tajwa wa usawa, tumejipanga kuchukua hatua kubwa mbalimbali ili kuwawezesha wanawake kuelekea malengo ya kutokomeza umaskini na njaa. Utafiti wa karibuni uliofanywa na shirika la FAO unaonyesha kuwa, wanawake wanaunda zaidi ya nusu ya nguvu kazi ya kilimo katika nchi nyingi chini ya Jangwa la Sahara, na pia chini ya nusu ya nguvu kazi katika nchi za kusini mashaŕiki mwa bara Asia.
Hii ni katika hali ambayo, katika mwaka wa kwanza wa janga la Covid-19 duniani, asilimia 22 ya wanawake walipoteza kazi na ajira zao katika sekta ya chakula na kilimo ikilinganishwa na asilimia 2 tu ya wanaume. Aidha wanawake walikabiliwa na uhaba wa chakula kuliko wanaume katika kipindi hicho".