China yaionya Marekani kuhusu mauzo ya silaha kwa Taiwan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i96532-china_yaionya_marekani_kuhusu_mauzo_ya_silaha_kwa_taiwan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, ameionya Marekani kuhusu kuendelea kuiuzia Taiwan silaha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2023 22:11 UTC
  • China yaionya Marekani kuhusu mauzo ya silaha kwa Taiwan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, ameionya Marekani kuhusu kuendelea kuiuzia Taiwan silaha.

"Wang Wenbin" alitangaza kuwa baadhi ya maafisa nchini Marekani wanatazamia kuitumia Taiwan kuidhibiti China, lakini wanapaswa kujua kwamba vitendo hivi ni hatari sana, na ni sawa na kucheza na moto. Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesisitiza kuwa, Beijing inataka Washington isitishe mauzo ya silaha na uhusiano wake na Taiwan na pia iheshimu kanuni ya China moja.

Onyo hili limekuja wakati ambapo habari kuhusu uamuzi wa Taiwan kununua makombora 400 ya Harpoon kutoka Marekani zikitangazwa kwenye vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Kulingana na tovuti ya habari ya Bloomberg, mnamo Aprili 7, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilisema kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba mkataba huo wa kuiuzia makombora Taiwan utagharimu dola bilioni 1.17,  na utakamilika  2029. Hii ina maana kwamba licha ya malalamiko ya China, Marekani bado inajaribu kuiuzia Taiwan silaha. Wakati huo huo, Taiwan yenyewe inajua kwamba katika mgogoro wowote utakaojiri kati ya kisiwa hiki na China, Taiwan haitaweza kukabiliana na mashambulizi makali ya China.

 Li Ming, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema: "Marekani huitumia Taiwan kwa njia mbili, kwanza, inaiona Taiwan kama soko zuri la kuuza silaha zake katika eneo hilo, na pili, Marekani inaitumia Taiwan kama njia ya kuishinikiza China. Wakati huo huo, Marekani inafahamu hisia za China katika suala hili, na inaonekana kwamba inapima kwa makusudi uvumilivu wa China kuhusu kadhia ya Taiwan.

Inavyoelekea ni kuwa, Marekani inafahamu matokeo ya mzozo wowote katika Mlango-Bahari wa Taiwan, na hivyo inatekeleza sera ya kichochezi lakini kwa njia ya kudhibiti hali ya mambo ili mgogoro mkubwa zaidi usiibuke. Lakini muelekeo huu haimaanishi kuwa China itakaa kimya na haitajibu vitendo vya uchochezi vya Marekani. Ingawa hapo awali, China ilipitisha sera ya subira ya kimkakati kuhusu uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Taiwan, lakini sasa imefikia natija kwamba kuendelea kwa sera hii kumewafanya wanaharakati wanaopigana kujitenga Taiwan wamepata kiburi na ujasiri zaidi kutokana na uungaji mkono wa Marekani.

 Kwa sababu hiyo, hivi karibuni China imeionya Marekani kwa  mazoezi yake kijeshi mtawalia baharini na angani na kwa njia hiyo kubainisha  kuwa subira yake inaweza kufika ukingoni kutokana na  harakati za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.

 "Henry Kissinger", mtaalam mwandamizi wa masuala ya kimataifa nchini Marekani  amoionya mara kadhaa Ikulu ya White House kuhusu matokeo ya kufika ukingoni subira na uvumilivu wa China kuhusu kadhia ya Taiwan. Kulingana na "Kissinger", Suala la Taiwan ni mstari mwekundu wa China na hivyo Marekani haiwezi kuvuka mstari huu bila woga. China imesisitiza mara kwa mara kwamba kamwe haiwezi kuligeza msimamo wake hata kidogo kuhusu mstari huu mwekundu."

Mashinikizo ya Marekani dhidi ya China yaliingia katika awamu mpya wakati wa urais wa Donald Trump.

Hivi karibuni, Trump aliashiria kudhoofika kwa dola ya Marekani mkabala wa Yuan ya China, na akasema hali hiyo ni sawa na Marekani kusindwa katika Vita vya Tatu vya Dunia.

Kwa hiyo, kwa kuzidisha mashinikizo dhidi ya China, serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden inajaribu kuficha kushindwa nchi hiyo katika sekta ya biashara mkabala wa China. Inavyoelekea ni kuwa China imeweza kusambaratisha sera za kivita za Marekani kuhusiana na Taiwan.

Hata hivyo, mvutano kati ya Marekani na China umekuwa ukiongezeka kila siku tangu ziara ya Spika wa zamani wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi nchini Taiwan. Licha ya China kupinga na kuonya mara kwa mara kuhusu safari kama hizo, wajumbe wa Marekani, wakiwemo wabunge na baadhi ya magavana wa majimbo, wamesafiri hadi Taiwan katika miezi ya hivi karibuni. Beijing imezitaja safari kama hizo kuwa za kichochezi na zenye lengo la kuingilia masuala ya ndani na kuwaunga mkono Wataiwan wanaotaka kujitenga na China.

Ingawa Taiwan imetawaliwa na serikali ya mitaa inayojitegemea tangu 1949, Beijing inakichukulia kisiwa hicho kama sehemu ya ardhi yake na inatekeleza hatua za kuhakikisha kuwa njia  za amani zinatumika kukiunganisha kisiwa hicho na China bara kama vilivyofanya kuhusu Hong Kong na Macau. Marekani na Umoja wa Ulaya zimekuwa zikifanya juu chini kuhakikisha kuwa Taiwan haiungani na China bara. Matamshi ya maafisa wa Ulaya kuhusu umuhimu wa kimkakati na kibiashara wa Taiwan kwa nchi za Magharibi ni dalili wazi kuwa madola hayo ya Magharibi yataendea kutekeleza sera za kichochezi kuhusu Taiwan.