Kuongezeka pakubwa gharama za maisha barani Ulaya
Kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali za mahitaji na gharama za maisha kunaendelea kuzitesa nchi mbalimbali barani Ulaya.
Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa, wananchi barani Ulaya wanalalamikia na ongezeko kubwa la bei za bidhaa za vyakula na kupanda kwa gharama za maisha.
Idara ya Takwimu ya Umoja wa Ulaya imeripoti kuwa, bei ya bidhaa za vyakula katika nchi za umoja huo ziliongezeka kwa asilimia 16.6 katika kipindi kilichoishia mwezi Aprili mwaka huu; kiwango ambacho kimetajwa kuwa cha juu juu zaidi ikilinganishwa na mfumuko wa bei cha asilimia 8.1. uliowahi kuripotiwa barani Ulaya katika kipindi sawa na hiki mwaka uliopita.
Makadirio ya karibuni aidha yanaonyesha kuwa, urithi wa mfumuko wa bei katika nchi za Ulaya umesababisha pigo kubwa kwa mapato ya kaya mbalimbali za wananchi barani Ulaya.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, mapato ya kaya mbalimbali barani Ulaya yalipungua kwa asilimia 6.5 katika ukanda wa Yuro baina ya mwaka 2020 na 2022 kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na nishati. Wakati huo huo madhara ya vita vya Ukraine kwa sekta za chakula, nishati na fedha pia yamekuwa yakiongezeka siku baada ya siku.