Watu 100 wapoteza maisha nchini China kwa kimbunga
Watu 100 wameripotiwa kupoteza maisha yao katika ajali ya upepo mkali ulioyakumba maeneo ya mashariki mwa China.
Taarifa zinaeleza kuwa, kimbunga hicho kimesababisha hasara kubwa ukiwemo uharibifu wa nyumba huku zaidi ya watu 800 wakijeruhiwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo upepo mkali uliokuwa ukienda kwa mwendo wa kilometa 125 kwa saa, umeukumba mji wa Yancheng na vijiji vya jirani na mji huo, katika mkoa wa Jieyang, mashariki mwa nchi hiyo. Rais Xi Jinping wa China sanjari na kuonyesha masikitiko yake juu ya tukio hilo la kimaumbile, amezitaka taasisi na mashirika husika kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kukabiliana na majanga kama hayo. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya vijiji ambavyo kimbunga hicho kimepitia, vimeharibiwa kabisa. Inaelezwa kuwa, huo ni upepo mkali kuwahi kuikumba nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 100 iliyopita. Afisa mmkoja wa mkoa wa Jieyang amenukuliwa akisema kuwa, shughuli za uokoaji, zimefanyika kwa mafanikio na kwamba tayari wameanzisha operesheni za usafishaji. Kadhalika serikali ya nchi hiyo imetuma zaidi ya polisi 300 katika mji huo kwa ajili ya kushiriki operesheni za usafishaji.